IQNA

Nukta kadhaa kuhusu uchaguzi wa Bunge wa Iraq

20:49 - October 13, 2021
Habari ID: 3474419
TEHRAN (IQNA)- Duru ya tano ya uchaguzi wa Bunge nchini Iraq imefanyika huku uchaguzi huo ukiibua maswali matatu makuu na ya kimsingi kuhusiana na uchaguzi huo.

Swali la kwanza ni kuwa, ushiriki mdogo wa wananchi wa Iraq katika uchaguzi huo ulikuwa na ujumbe gani? Swali pili, kwa nini harakati ya Sadr imefanikiwa kupata viti vingi vya Bunge na kuiacha kwa mbali mirengo mingine katika uchaguzi huo? Ama swali la tatu ni kuwa, kwa nini asilimia 29 ya viti vya Bunge vimechukuliwa na wanawake?

Uchaguzi wa Bunge nchini Iraq ulifanyikka Jumapili iliyopita ya tarehe 10 Oktoba. Tukitupia jicho takwimu za uchaguuzi huo tunakutana na nukta kadhaa muhimu. Takwimu rasimu zinaonyesha kuwa ushiriki wa wananchi katika uchaguzi huo ulikuwa ni asilimia 41. Hata hivyo takwimu zisizo rasmi zinaonyyesha kuwa, ushiriki huo ulikuwa mdogo zaidi na zinasema kwamba, ulikuwa ni wa asilimia 39. Pamoja na yote hayo, hata ikiwa ni kweli kwamba, ushiriki huo ulikuwa ni wa asilimia 41 bado ni wa chini mno ikilinganishwa na duru zilizotangulia za uchaguzi wa Bunge nchini humo. Kwa msingi huo basi, panajitokkeza swali muhimu ambalo ni kwa nini asilimia 60 ya wananchi wa Iraq hawakushiriki katika uchaguzi wa Bunge wa Jumapili?

Ili kujibu swali hili tunapaswa kurejea matukio ya maandamano na malalamiko ya Oktoba 2019, malalamiko ambayyo yalipelekea kuanguka serikali ya Waziri Mkuu Adel Abdul-Mahdi. Chimbuko la malalamiko hayo lilikuwa ni kutoridhishwa wananchi wa Iraq na hali mbaya ya uchumi, huduma mbovu na duni za kijamii na kulalamikia ufisadi uliokithiri katika nchi hiyo ya Kiarabu. Katika kipindi cha mwaka mmoja na nusu uliopita, hali ya kiuchumi ya wananchi pamoja na huduma za kijamii ni vitu ambavyo havijaboreka kabisa.

Kwa msingi huo, wananchi wa Iraq wameonyesha malalamiko yao na kutoridhishwa na utendaji wa serikali kwa kutoshiriki katika uchaguzi huo wa Bunge. Ujumbe wa asilimia 60 ya Wairaqi ambao hawajashiriki katika uchaguzi wa Jumapili ni kuwa, hawaridhwishi na hali ilivyo hivi sasa, na hivyo wanasiasa wa nchi hiyo wanapaswa kutafuta dawa mujarabu ili kubadilisha mtazamo huu wa wananchi na hivyo kuzuia malalamiko hayo yasibadilike na kuwa hali ya kukata tamaa.

Kuhusiana na hilo, Shirika la Habari la Ufaransa AFP limeashiria katika ripoti yake suala la kupungua ushiriki wa wananchi wa Iraq katika uchaguzi wa Bunge na kueleza kwamba, miongoni mwa sababu ya hilo ni malalamiko ya wananchi dhidi ya jinamizi la ufisadi linaloisumbua nchi hiyo.

Matokeo ya uchaguzi wa Bunge nchini Iraq yanaonyesha kuwa, Muungano wa Sairoon (Sairoon Alliance) wenye mfungamano na Harakati ya Sadr umejinyakulia viti 73 ambavyo ni takribani mara mbili ya  vita vya Bunge vya Muungano wa Taqaddum (Taqaddum Coalition) unaoongozwa na Spika wa Bunge Mohammed al-Halbousi ambao umepata viti 38.  Katika uchaguzi wa mwaka 2018, Harakati ya Sadr inayoongozwa na Sayyid Muqtada Sadr ilipata viti 54 vya Bunge. Hivyo basi, swali jingine muhimu hapa ni kuwa, nini kimepelekea mrengo wa Sadr ufanikiwe kuibuka kidedea na kuipiku mirengo mingine ya kisiasa katika uchaguzi wa mara hii?

Wachambuzi wa masuala ya Iraq wanaamini kuwa, ushiriki mdogo wa wananchi katika uchaguzi wa mara hii umekuwa kwa manufaa wa Harakati ya Sadr; kwani mrengo huu ulikuwa umejipanga na kuwa na mshikamano zaidi ikilinganishwa na miungano mingine. Kiujumla ni kuwa, kadiri ushiriki unapokuwa mdogo, basi muungano ambao umejipanga na kuwa na mshikamano zaidi ndio unaoweza  kufanikiwa katika uchaguzi. Hali hii ilishuhudiwa dhahir shahir kwa Harakati ya Sadr.

Takwimu nyingine muhimu za uchaguzi huo zilizotolewa baada ya kura kuhesabiwa zinaonyesha kufanikiwa wanawake kupata viti 97 vya Bunge. Kwa mujibu wa sheria za uchaguzi, wanawake wametengewa kwa akali viti 83 vya Bunge. Bi Yusra Karim Muhsin, Mkurugenzi wa Idara ya Uwezeshaji Wanawake Katika Sekretarieti ya Serikali ya Iraq anasema kuwa, kwa mujibu wa tathmini za awali za uchaguzi huo wa Bunge, wanawake wamefanikiwa kupata viti 97 ikiwa ni viti 14 zaidi ya hisa maalumu waliotengewa na Bunge kwa mujibu wa sheria.

Hata hivyo jambo muhimu kama alivyosema Bi Yusra Karim Muhsin ni kuwa, matokeo hayo yanaonyesha kuwa, wanawake 57 wameshinda viti vya Bunge kwa kura nyingi bila ya kutegemea hisa ya wanawake. Kwa maneno mengine ni kuwa, wanawake 57 walifanikiwa kuwabwaga wanaume waliochuana nao katika katika kinyang'anyiro cha kuwania viti vya Bunge. Hili linaweza kuwa na ujumbe huu kwamba, sehemu ya kura za Wairaqi kwa wanawake ni ishara ya kulalamikia utendaji wa serikali katika miaka ya hivi karibuni. Kwa msingi huo basi, serikali ijayo ya Iraq itakuwa na kibarua kigumu; kwani inapaswa kuyapa umuhimu na kusikiliza malalamiko ya wananchi wa nchi hiyo.

4004711

Kishikizo: iraq uchaguzi
captcha