IQNA

Watu 6 wauawa baada ya kufyatuliwa risasi katika maandamano Beirut

19:08 - October 14, 2021
Habari ID: 3474422
TEHRAN (IQNA)- Duru za habari nchini Lebanon zimeripoti kuwa mapigano makali yanendelea baina ya askari usalama na watu wasiojulikana katika mji mkuu wa Lebanon, Beirut ambapo idadi ya waliouawa sasa ni sita na waliojeruhiwa ni zaidi.

Kwa mujibu wa televisheni ya Al Manar imesema watu hao sita wameuawa shahidi kwa kupigwa risasi na wanamgambo wasiojulikana wakati wakiwa katika maandamano ya amani  kuhusiana na uchunguzi wa mlipuko wa mwaka jana mjini Beirut.

Baadhi ya duru zinasema mauaji hayo yametekelezwa na kundi la wanamgambo Wakristo linalojulikana kama Lebanese Forces Party.

Duru za habari nchini Lebanon zimetangaza kuwa, sauti za milio ya risasi na mifyatuo ya roketi imesikika katika eneo la At-T'ayyunah mjini Beirut ambako mapigano yanaendelea baina ya pande mbili.

Kanali ya Al Mayadeen imezinakili duru za tiba na kuripoti kuwa idadi ya watu waliofariki imefikia sita na majeruhi wamepindukia watu 60.

Vyombo vya habari vya Lebanon vimeripoti pia kuwa, jeshi la nchi hiyo linaendelea kupeleka askari na zana za kijeshi eneo la mapigano na kwamba magari ya deraya yamesambazwa maeneo ya Ash-Shayah na A'inur-Ramaanah sambamba na kuwaondoa raia katika maeneo hayo.

Waziri wa Mambo ya Ndani wa Lebanon Bassam Mawlawi amesema katika mkutano aliofanya na waandishi wa habari mapema leo kwamba mapigano yalianza baada ya wadunguzi kadhaa kuwafyatulia risasi raia. Mawlawi amesisistiza ulazima wa kuchukuliwa hatua za lazima kulinda harakati za amani za kiraia na kuwatia nguvuni watu wanaobeba silaha.

Mapigano mjini Beirut yalianza baada ya duru za habari za Lebanon kuripoti leo asubuhi kuwa, waungaji mkono wa Hizbullah na harakati ya Amal wamejitokeza mabarabarani katika maandamano ya amani kulalamikia utendaji wa Tariq Bitar, mchunguzi mkuu wa faili la mripuko wa bandari ya Beirut.

Muda mfupi baada ya kutangazwa habari hiyo, vyombo vya habari viliripoti kuwa umetokea ufyatuaji risasi zilizolenga raia na kujeruhi watu kadhaa.

/4004901

Kishikizo: lebanon Beirut bandari
captcha