IQNA

Wapalestina wapongeza Malaysia kwa kukataa kuanzisha uhusiano na utawala wa Israel

16:38 - October 21, 2021
Habari ID: 3474451
TEHRAN (IQNA)- Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (Hamas) imepongeza tamko la Waziri wa Mambo ya Nje wa Malaysia ambaye amesema nchi yake katu haitaanzisha uhusiano na utawala wa Kizayuni wa Israel.

Katika taarifa leo Alhamisi, Hamas imepongeza tamko la Saifuddin Abdullah, Waziri wa Mambo ya Nje wa Malaysia ambaye amekanusha madai ya utawala wa Kizayuni wa Israel kuwa eti Malaysia imeazimia kuanzisha uhusiano na utawala huo.

Hamas imemshukuru waziri huyo wa mambo ya nje wa Malaysia kutokana na msimamo wake wa kusimama pamoja na taifa la Palestina kwa ajili ya mapambano dhidi ya utawala wa Kizayuni wa Israel.

Siku ya Jumatano Waziri wa Mambo ya Nje wa Malaysia alisisitiza kuwa nchi yake itaunga mkono mapambano ya kupigania ukombozi wa Palestina na itaendelea kupinga kitendo cha Israel kuendelea kukalia kwa mabavu ardhi za Palestina.

Abdullah aidha amepinga madai ya utawala wa Kizayuni kuwa yamkini Malaysia ikatia saini mapatano ya kuanzisha uhusiano na utawala wa Kizayuni kama zilivyofanya Morocco, Bahrain, Sudan na Umoja wa Falme za Kiarabu mwaka jana.

Hivi karibuni Issawi Frej Waziri wa Ushirikiano wa Kieneo wa utawala wa Kizayuni wa Israel alidai kuwa Oman, Tunisia, Qatar na Malaysia ziko tayari kutia saini mapatano ya kuanzisha uhusiano wa kawaida na utawala huo ghasibu.

4006897/

captcha