IQNA

Wanazuoni wa Kiislamu watakiwa wazuie mifarakano baina ya Waislamu

17:40 - October 21, 2021
Habari ID: 3474452
TEHRAN (IQNA)- Mwanazuoni mwandamizi wa Iraq amesisitiza kuhusu ulazima wa wanazuoni na maulamaa wa Kiislamu dunaini kuwa macho ili kuzuia njama za maadui za kuchochea mifarakano baina ya Waislamu.

Katika mahojiano na IQNA pembizoni mwa kongamano la 35 la kimataifa la Umoja wa Kiislamu ambalo linaendelea Tehran kwa mnasaba wa Wiki ya Umoja wa Kiislamu, Sheikh Khaled al Mulla amesisitiza kuhusu udharura na umuhimu wa umoja wa Waislamu.

Sheikh al Mulla ambaye pia ni mwenyekiti wa Jumuiya ya Maulamaa wa Ahul Sunna Iraq amesema maadui wa Uislamu kwa kuunga mkono makundi yenye misimamo mikali ya kidini ambayo wanalenga kuibua mifarakano na kuvuruga umoja wa Kiislamu na hivyo maulamaa wana jukumu nzito katika kukabiliana na njama hizi.

Mwanazuoni huyu wa Iraq anasema kuwepo mitazamo tafauti baina ya mafuqaha na maulamaa pamoja na kuwepo madhehebu kadhaa ni chanzo za nguvu za umma wa Waislamu lakini maadui wa Uislamu wanatumia mbinu mbali mbali kuleta mifarakani baina ya wafuasi wa madhehebu za Shia na Sunni.

Mkutano wa 35 wa Kimataifa wa Umoja wa Kiislamu ulianza Jumanne hapa mjini Tehran kwa kaulimbiu ya "Umoja wa Kiislamu; Amani na Kuepukana na Mifarakano na Mizozo" kwa hotuba ya Rais Ebrahim Raisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

Mkutano huo wa siku tano, ambao kwa sababu ya kuchunga miiko na miongozo ya kiafya ya kujiepusha na janga la corona unafanyika kwa mahudhurio ya moja kwa moja na kwa njia ya intaneti, unahudhuriwa na washiriki kutoka Iran na nchi 39 duniani.

Inafaa kuashiria hapa kuwa, Tuko katika siku tukufu za kuadhimisha Maulid ya Mtume Mtukufu wa Uislamu Mohammad al Mustafa SAW, siku ambazo ni maarufu kama Maulidi. Waislamu wa madhehebu ya Sunni wanaadhimisha siku hiyo tarehe 12 Rabiul Awwal na Waislamu wa Madhehebu ya Shia wanamini siku hiyo ni tarehe 17 Rabiul Awwal.

Miaka mingi iliyopita, Hayati Imam Khomeini MA, Kiongozi mwanzilishi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran, ambaye binafsi alikuwa mstari wa mbele kulingania umoja wa Kiislamu alipendekeza kuwa, muda uliopo baina ya tarehe hizo mbili uwe ni "Wiki ya Umoja wa Waislamu" kwa lengo la kuimarisha mashikamano na udugu baina ya madhehebu za Kiislamu.

4004073

captcha