IQNA

Mashindano ya Qur’an ya wanawake yafanyika Tanzania

16:54 - October 23, 2021
Habari ID: 3474459
TEHRAN (IQNA) - Kina mama wa Kiislamu wametakiwa kuongeza juhudi katika kutimiza jukumu la kuandaa watoto wao kutokana na kukithiri kwa mmomonyoko wa maadili, kwani watoto wema na bora wanaanza na wazazi bora hasa kina mama.

Hayo yameelezwa na Mbunge wa Viti Maalumu mkoa wa Dar es salaam Mh. Mariam Kisangi, alipomwakilisha mgeni rasmi Mh. Salma Kikwete, ambaye alitarajiwa kuwa mgeni rasmi katika mashindano ya wanawake ya kuhifadhi Qur`an mkoa wa Dar es Salaam, yaliyoandaliwa na Taasisi ya Bi. Aisha Sururu ambayo yalifanyika hivi karibuni.

Mhe. Kisangi alisema kuwa maadili bora katika familia yanapatikana kwa kuwapatia watoto elimu bora ya Dini na sekula na kwamba, watoto wakipatiwa elimu sahihi hasa kuhusu imani yao, hawatofanya mambo ya yasiyompendeza Mola wao na kuwa kizazi chema.

“Niwaombe wazazi wenzangu na kina mama kwa ujumla, tufanye kila linalowezekana kuawaandaa watoto wetu katika maadili mazuri yanayokubalika katika jamii, ili kuisaidia nchi hii kuwa sehemu salama ya kuishi” Alisema Mh. Kisangi.

Aidha kina mama hao wamekumbushwa kumuombea dua Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mama Samia Suluhu Hassani, kwa kazi kubwa na nzito ya kuliongoza taifa, kwani wao kina mama wanaweza kutambua kwa urahisi majukumu mazito yanayomkabili Rais kupitia namna wanavyopambana kuzilea familia zao.

“Tizameni namna tunavyopambana, huyu Mh. Rais yeye ni wa nchi nzima, tujiulize majukumu yanayomkabili, hivyo ni jukumu letu kina mama kumsaidia mwenzetu huyu kwa kumuombea dua, ili iwe rahisi kwake kwa msaada wa Mwenyezi Mungu kuiongoza nchi hii kwa salama na amani”, alifafanua Mh. Kisangi.

Fainali ya mashindano ya 10 ya kuhifadhi Qur’an tukufu kwa wanawake watu wazima mkoa wa Dar es Salaam, yameandaliwa na Aisha Sururu Foundation na kufanyika kwa mafanikio makubwa.

Kwa upande wake Bi. Sururu, amesema kuwa lengo na dhumuni la kufanya mashindano hayo ni kuwainua wanawake kiuchumi, lakini pia kuwafanya waipende na waisome Qur’an kwani ndio muongozo wa Waislamu.

Bi. Sururu ambaye ni Mwenyekiti wa taasisi ya Aisha Sururu, amesema kuwa mashindano ya mwaka huu yalikuwa ya aina yake ambapo wameshiriki kina mama wa umri mkubwa, ili kudhihirisha kuwa kina mama na wanawake kwa ujumla wanatakiwa kuiishi Qur’an, kwani mtu akishikamana na Qur’an hawezi kuishi katika mambo maovu na yakumchukiza Allah (SWT).

Aidha amewataka kina mama kujishughulisha na shughuli za kujipatia kipato chao cha halali, kwani kina mama wakifanikiwa katika familia, ni mwanzo wa familia hiyo kuondokana na maisha ya dhiki.

“Kina mama msiache kushiriki katika shughuli mbalimbali za kiuchumi, nendeni mkajishughulishe ili familia zenu ziondokane na unyonge kwani familia ikiwa haina kipato kizuri, watoto wanakuwa wanyonge na kukosa raha” alisema Bi. Sururu.

Pia amewataka kina mama wasijibweteke na kujiona kuwa umri wao umeenda hivyo hawana nafasi ya kujiendeleza katika mafunzo ya Qur’an na ujasiria mali. Aliwataka kuisoma dini yao ili wawe walezi bora katika familia zao kwani familia ikiwa na mama mwenye dini inakuwa bora.

Annnur Tanzania

 

captcha