IQNA

Rais wa Iran katika mazungumzo ya simu na Rais wa Ufaransa

Mazungmzo ya nyuklia Vienna yahitimishwe kwa Iran kuondolewa vikwazo

20:14 - November 30, 2021
Habari ID: 3474622
TEHRAN (IQNA)- Rais Ibrahim Raisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amemfahamisha Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa kuwa, Iran inataka kuona natija katika mazungumzo ya nyuklia yanayoendelea sasa Vienna Austria na kwamba lazima mazungumzo hayo yahitimishwe kwa Iran kuondolewa vikwazo.

Raisi ametoa tamko hilo Jumatatu  baada ya Macron kumpigia simu ambapo mazungumzo yao yaliyendelea kwa muda wa saa moja na nusu.

Katika mazungumzo hayo, marais hao wawili walijadili hali ya mambo katika mazungumzo ya Vienna kuhusu kuondolewa vikwazo dhidi ya Iran na pia wamejadili masuala yenye umuhimu kwa pande mbili. Rais wa Iran amesema vikwazo  havijaweza kuzuia ustawi wa Iran na leo dunia inafahamu ni nchi gani iliyokiuka mapatano ya JCPOA na hivyo mkiukaji wa mapatano hayo anapaswa kutekeleza ahadi zake.

Aidha amesema hali ya sasa imetokana na Marekani na nchi za Ulaya kutotekeleza ahadi zao katika mapatano ya JCPOA.

Raisi amemtaka Macron ashirikiane na washiriki wengine wa mazungumzo ya Vienna ili vikwazo dhidi ya Iran viondolewe.

Kwa upande wake Macron amelaani hatua ya Marekani kujiondoa katika mapatano ya JCPOA na kusema nchi yake inaamini kuwa kulinda mapatano hayo ni jukumu la nchi zote zilizoyaafiki. Amesema tayari ameshazungumza na Rais Joe Biden wa Marekani kuhusu kadhia hiyo.

Mazungumzo hayo yamekuja baada ya duru mpya ya mazungumzo kufanyika Vienna jana baina ya Iran na nchi za kundi la 4+1 kuhusu kuondolewea vikwazo vya Marekani dhidi ya Iran. Nchi za 4+1 ni China Russia, Ufaransa, Uingereza, Ujerumani pamoja na mwakilishi wa Umoja wa Ulaya. Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Ali Baqeri aliyeoongoza timu ya mazungumzo amesema pande zote zimeafiki kujikita katika kuondolewa vikwazo ambavyo viliwekwa na Marekani mwaka 2018 baada ya Washington kujiondoa katika mapatano ya JCPOA.

/3483595

captcha