Katika azimio ambao limepitishwa leo, Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa limeeleza kuwa, uamuzi uliochukuliwa na Israel Disemba 14 mwaka 1981 wa kulazimisha sheria na kuamua kuikalia kwa mabavu Miinuko ya Golan huko Syria ni batili, usio na itibari na kinyume cha sheria.
Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa limesema:"Kama ambavyo Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lilivyosisitiza katika azimio nambari 497 la mwaka 1981, Israel inapaswa kukomesha hatua zake na kuondoka kikamilifu katika eneo linalokaliwa kwa mabavu la Miinuko ya Golan tarehe 4 Juni mwaka 1967."
Nchi 94 wanachama wa Umoja wa Mataifa zimepiga kura ya ndiyo kwa azimio hilo la Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa.
Mwakilishi wa kudumu wa Syria katika Umoja wa Mataifa Bassam Sabbagh amehutubia kikao hicho cha Baraza Kuu la UN na kusema mwenendo wa sasa wa Umoja wa Mataifa wa kutotekeleza maazimio yake unaushajiisha utawala ghasibu wa Israel kuendeleza uvamizi na ukanzamizaji dhidi ya raia wa Syria katika eneo linalokaliwa kwa mabavu la Golan.