IQNA

Kikao cha kumuenzi Marhum Qarii El-Minshawi kupitia intaneti + Video

21:23 - January 19, 2022
Habari ID: 3474828
TEHRAN (IQNA)- Kikao cha kumuenzi qarii maarufu wa Misri Marhum Mohammad Siddiq El-Minshawi kimefanyika kwa njia ya intaneti kwa hisani ya Shirika la Habari za Qur'ani la Kimataifa (IQNA) na Taasisi ya Iran ya Ahsan ul Hadith.

Kikao hicho kimefanyika Jumatano alasiri kwa mnasaba wa maadhimisho ya mwaka wa 102 tokea alipozaliwa Marhum Minshawi.

Wanaharakati wa Qur'ani kutoka Iran na maeneo mengine duniani wameshiriki katika kikao hicho kwa njia ya video ambao wamezungumza kitaalamu kuhusu usomaji Qur'ani Tukufu wa qarii huyo bingwa wa Misri.

Kati ya walioshiriki katika kikao hicho ni qarii mkongwe wa Iran Seyed Mohsen Mousavi Baladeh, Mkuu wa Taasisi ya Qur'ani ya Lebanon Talal al-Masar, qarii maarufu wa Lebanon Hussain Hamdan, qarii maarufu wa Iraq Yahya al-Sahaf na qarii kutoka Syria Rizwan Darwish.

Mohammad Siddiq El-Minshawi ni maarufu kwa sauti yake yenye mvuto.

El-Minshawi alizaliwa Januari 1920 katika mji wa Al Minshah katika jimbo la Sohag nchini Misri na alilelewa na kuinukia katika familia ya wasomaji Qur'ani. Alifanikiwa kuhifadhi Qur'ani Tukufu kikamilifu akiwa na umri wa miaka 8 na mwaka mmoja baadaya akaanza kujifunza kusoma Qur'ani kitaalamu.

Baada ya muda usio mrefu Minshawi alipata umashuhuri kama qarii ambaye alikuwa akitumia mbinu za Tarteel na Tahqiq katika usomaji wake. Alisafiri katika nchi nyingi duniani kwa ajili ya usomaji Qur'ani zikiwemo Indonesia, Jordan, Saudi Arabia, Syria, Iraq, Pakistan na Sudan. Aliaga dunia mwaka 1969 akiwa na umri wa miaka 49.

Misri ni mashuhuri duniani kama nchi ambayo imeweza kutoa wasomaji bora zaidi wa Qur'ani Tukufu katika miongoi ya hivi karibuni.

Hii hapa chini ni moja ya klipu za qiraa ya Marhum El Minshawi.

3948722/

captcha