IQNA

Kongamano la Karbala lapendekeza kuundwa Jumuiya ya Kimataifa ya Qur’ani

20:13 - January 21, 2022
Habari ID: 3474834
TEHRAN (IQNA)- Kongamano la kimataifa la kujadili mfumo na nidhamu ya pamoja ya majaji wa mashindano ya kimataifa ya Qur’ani limemalizika Alhamisi katika mji wa Karbala nchini Iraq.

Taarifa ya mwisho ya kongamano hilo imetoa wito wa kuundwa Jumuiya ya Kimataifa ya Qur’ani Tukufu.

Wawakilishi wa nchi 16, ikiwemo Jamhuri ya Kiislamu ya Iran wameshiriki katika kikao hicho cha kimataifa ambacho kimeandaliwa na Kituo cha Darul Qur’ani cha Ofisi ya Mfawidhi wa Haram ya Imam Hussein AS.

Afisa wa kituo hicho, Safa al Silawi, amesema taarifa ya mwisho ya kikao hicho imesomwa na Rafi al-Ameri qarii na mtaalamu mwandamizi wa Qur’ani Tukufu nchini Iraq ambaye pia ni mkurugenzi wa Kituo cha Kitaifa cha Sayansi za Qur’ani Iraq.

Taarifa hiyo imesisitiza kuhusu haja ya kuundwa jumuiya ya kimataifa ya Qur’ani Tukufu ili kusaidia utekelezwaji wa yale yaliyopitishwa katika kongamano hilo.

Silawi amesema vigezo vya majaji wa mashindano ya Qur’ani ambavyo vimeidhinishwa katika kongamano hilo vitawasaidia sana wanaohifadhi na kusoma Qur’ani na hivyo kuleta nidhamu ya pamoja itakayotumiwa na majaji wote wa mashindano ya kitaifa na kimataifa ya Qur’ani Tukufu.

Aidha amesema kongamano lijalo kama hilo la Karbala linaweza kuandaliwa na nchi zingine za Kiislamu kwa ushirikiano na Kituo cha Darul Qur’an.

Kongamano hilo lilianza Jumatatu katika Chuo Kikuu cha Al Zahra mjini Karbala.

Wawakilishi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika kongamano hilo la kimataifa walikuwa ni Seyed Abbas Anjam Mehdi Qarasheikhlu, Gholam Reza Shahmiveh, Mohammad Rasoul Abaei, Shahriari Parhizgar na Mehdi Daqaqeleh ambao wote ni wataalamu bingwa wa Qur’ani Tukufu.

 
 

4030115

captcha