IQNA

Katibu Mkuu UN alaani mauaji ya Saudia dhidi ya raia nchini Yemen

17:15 - January 22, 2022
Habari ID: 3474837
TEHRAN (IQNA)- Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amelaani mashambulizi ya ndege za kivita za Saudi Arabia dhidi ya jela ya wafungwa katika mkoa wa Sa'ada nchini Yemen.

Taarifa iliyotolewa na Antonio Guterres imesema shambulizi jingine limesajiliwa nchini Yemen  ambalo limeua raia wakiwemo watoto wadogo.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ametoa wito wa kufanyika uchunguzi wa haraka na wa wazi kuhusu mashambulizi hayo na kuwawajibishwa wahusika.

Vilevile ametoa wito wa kukomeshwa mzingiro wa Saudia na washirika wake dhidi ya bandari na viwanja vya ndege vya Yemen na kuanzishwa tena mazungumzo ya kutafuta suluhisho la mgogoro wa nchi hiyo. 

Mashambulizi ya anga yaliyofanywa na ndege za kivita za Saudia dhidi ya jela ya mkoa wa Sa'ada huko Yemen yametajwa kuwa miongoni mwa mashambulizi yaliyosababisha maafa makubwa ya raia.

Takwimu za karibuni zinasema watu wasiopungua 77 wameuawa katika hujuma hiyo ya kinyama ya ndege za kivita za utawala wa kifalme wa Saudi Arabia na wengine zaidi ya 140 wamejeruhiwa. 

Wakati huo huo,

Msemaji wa Jeshi la Yemen ameyashauri makampuni ya kigeni ya uwekezaji kuondoka Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE).

Kwa mujibu wa shirika la habari la Fars, Yahya Saree, msemaji wa Jeshi la Yemen ametoa taarifa akisema kuwa baada ya ukatili uliofanywa na jeshi la anga la muungano wa Saudia, Marekani na Imarati dhidi ya watu wa Yemen, tunayashauri makampuni kigeni kuondoka katika nchi ndogo ya UAE.

Brigedia Saree amesisitiza kwamba, maadamu watawala wa Imarati wanaendelea na uchokozi wao dhidi ya Yemen, hii itakuwa na maana kwamba makampuni ya kigeni yaliyowekeza katika nchi hiyo ndogo hayatakuwa salama.

Matamshi hayo ya msemaji wa Jeshi la Yemen yametolewa kufutia hujuma kubwa ya ndege za kivita za Saudi Arabia iliyolenga makazi na raia na jela la mkoa wa Sa'ada. 

Kufuatia shambulio hilo la kinyama la ndege za kivita za Saudi Arabia, dhidi ya maeneo ya raia huko Yemen, Muhammad Ali al-Houthi, mjumbe wa Baraza Kuu la Kisiasa la nchi hiyo amesema, hujuma hiyo ni "jinai ya kivita" na "haisameheki."

Amesema wananchi shupavu wa Yemen watatoa majibu makali na kwa nguvu zote dhidi ya madola vamizi yanayoongozwa na utawala wa wa Saudi Arabia.

/84621971

captcha