IQNA

Serikali ya Iran inataka kuwa na uhusiano na dunia nzima

19:03 - January 26, 2022
Habari ID: 3474855
TEHRAN (IQNA)- Rais Ebrahim Raisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema serikali yake inalenga kuwa na ushirikiano na dunia nzima lakini akaonya kuwa Iran itakabiliana na madola yanayotaka kukabiliana na nchi hii.

Raisi amesema hayo Jumanne usiku alipozungumza na taifa kupitia mahojiano ya moja kwa moja ya televisheni ambapo ameongeza kuwa serikali ya awamu ya 13 inafuatilia suala la kuwa na uhusiano na mataifa yote ya dunia yanayotaka kuwa na uushirikiano na Tehran. Hata hivyo Rais wa Iran ameonya kwamba, yale mataifa yanayolenga kukabiliana na Iran basi Tehran nayo itasimama kukabiliana nayo.

Rais Raisi ameendelea kubaini kuwa, endapo pande husika katika makubaliano ya nyuklia ya JCPOA zitakuwa tayari kuliondolea vikwazo vya kidhalimu taifa hili, basi kuna uwezekano wa kufikiwa aina yoyote ya makubaliano kamili.

Aidha amebainisha kwamba, matokeo ya safari na mazungumzo na viongozi wa mataifa mbalimbali yanapaswa kudhamini maslahi ya taifa hili, kupanuliwa wigo wa ustawi katika nyanja mbalimbali na kwamba, kutoa tabasamu tu bila ya kuweko matunda na matokeo ni jambo lisilo na faida yoyote kwa wananchi.

Rais Ebrahim Raisi amesisitiza kuwa, kama katika mazungumzo yanayoendelea hivi sasa huko Vienna Austria pande husika zitakuwa tayari kuliondolea vikwazo vya kidhalimu dhidi ya taifa la Iran, basi kuna mazingira na uwanja wa kufikiwa makubaliano.

Akijibu swali kuhusiana na jinsi mazungumzo ya Vienna yanayoendelea na kwamba, msimamo wa Iran ni upi ikiwa Marekani itataka kufanya mazungumzo ya moja kwa moja na taifa hili, Rais Ebrahim Raisi amesema, kwa muda sasa Washington imekuwa ikitoa ombi hilo lakini hadi sasa mazungumzo hayo hayajafanyika.

4031373

captcha