IQNA

Watoto na Qur'ani

Watoto wa Misri wakaribisha kuanzishwa tena masomo ya Qur'ani Misikitini

18:02 - May 25, 2022
Habari ID: 3475292
TEHRAN (IQNA) - Usajili wa masomo ya Qur'ani Tukufu katika majira ya joto katika misikiti ya Misri umepokelewa vyema na watoto wa shule.

Wizara ya Wakfu ya nchi hiyo ilisema wiki iliyopita kwamba baada ya miaka miwili ya kusimamishwa kutokana na janga la corona, usajili umeanza kwa masomo ya Qur'ani ya majira ya joto misikitini.

Tangu kutangazwa kuanza zoezi la uandikishaji, idadi kubwa ya wanafunzi wa shule wamejiandikisha kwa ajili ya kozi na programu za Qur'ani Tukufu.

Katika uchunguzi uliofanywa na wizara hiyo, wazazi walisema watoto wao wana furaha kubwa kuweza kurejea misikitini kwa ajili ya elimu ya Qur'ani tena pamoja na shughuli zingine za kidini na kitamaduni.

Masomo ya Qur'ani ya majira ya joto  yanalenga kuinua mwamko wa kidini miongoni mwa watoto wa shule na kuwaepusha na itikadi kali, kwa mujibu wa Waziri wa Wakfu Wa Misri Sheikh Mohamed Mukhtar Gomaa.

Waziri Gomaa alisema kulea watoto kwa kuzingatia maadili na akhlaqi njema pamoja na utamaduni wenye busara ni miongoni mwa haki zao.

Misri ni nchi ya Afrika Kaskazini yenye wakazi wapatao milioni 100. Waislamu ni takriban asilimia 90 ya watu wote wa nchi hiyo.

Shughuli za Qur'ani Tukufu ni mashuhuri  sana katika nchi  hii ya Kiarabu yenye wasomi wengi wa Qur'ani Tukufu.

 

4059593

captcha