IQNA

Waislamu Kanada

Mji Kanada kujenga Msikiti ili kuwashawishi madaktari Waislamu wabaki

23:04 - August 18, 2022
Habari ID: 3475643
TEHRAN (IQNA) – Mji wa Gander katikati mwa jimbo la Newfoundland na Labrador nchini Kanada (Canada) unafanya kazi na jumuiya yake ya Waislamu wa eneo hilo kuanzisha msikiti wake wa kwanza ili kuwashawishi madaktari Waislamu wasihame eneo hilo.

Meya wa Gander Percy Farwell na Dk. Mohamed Barasi, mkurugenzi wa Jumuiya ya Kiislamu ya Central Newfoundland, wamesema wanatumai ujenzi wa msikiti utakuwa ni motisha kwa madaktari Waislamu kusalia katika eneo hilo.

Farwell anasema kuna madaktari kadhaa Waislamu wanaofanya kazi Gander, na kwamba huko nyuma, mji huo umekuwa na matatizo ya kuwashawishi kubaki. Huku akipongeza juhudi za serikali ya mkoa kuwavutia wahitimu wa kimataifa wa udaktari, alisema jamii zinazohitaji utaalamu wao zina jukumu muhimu katika kuwahifadhi.

"Madaktari ni sehemu ya familia, na familia zina mahitaji ambayo yako nje ya maisha ya kitaalam ya daktari," Farwell alisema na kuongeza kuwa jamii inapaswa kukidhi mahitaji ya madaktari.

Kama ilivyo kwa jimbo la Newfoundland na Labrador, mji  wa Gander unahitaji madaktari zaidi, Farwell alisema. Katika jimbo lenye watu wapatao 522,875, karibu robo hawana daktari wa familia, Chama cha Madaktari cha Newfoundland na Labrador kimesema.

Barasi, daktari wa upasuaji wa mifupa, alisema jumuiya yake imekuwa ikifanya kazi na mji wa Gander kwa zaidi ya mwaka mmoja kuanzisha msikiti na tayari wamegundua eneo linalofaa la ardhi.

Alisema kwa sasa wako katika mchakato wa kuandaa makaratasi ya kujiimarisha kama shirika la hisani lililosajiliwa ili kuanza kukusanya fedha za kununua ardhi hiyo.

Gander ina idadi ya watu wapatao 11,600 na kuna hospitali ya mkoa yenye shughuli nyingi na kituo cha afya. Farwell anakadiria Waislamu wa eneo hilo kuwa ni 55, lakini anasema idadi hiyo inakaribia 100 ikiwa jumuiya zinazozunguka zitajumuishwa.

Barasi alisema msikiti wa eneo hilo utasaidia hitaji muhimu kwa Waislamu huko Gander, pamoja na wale walio katika jamii za karibu.

"Kama wewe ni daktari Mwislamu unafanya kazi Newfoundland, mhitimu wa kimataifa - baada ya miaka miwili au mitatu, ikiwa unaweza kwenda Ontario kwa sababu mshara ni ule ule," Barasi alisema. "Utapata misikiti mingi huko, na unaweza kwenda msikitini badala ya kukaa nyumbani. Unaweza kutekeleza mafundisho ya kidini.”

Wakati wa Mwezi Mtukufu wa Ramadhani mwaka huu, mji uliruhusu Jumuiya ya Kiislamu ya Newfoundland kukusanyika katika jengo kwenye bustani ya jiji, Farwell alisema.

Dk. Nizar Belgasem, daktari ambaye amekuwa akifanya kazi huko Gander tangu 2017 kabla ya kuchukua likizo ya muda kwa mafunzo zaidi, alisema mjumuiko huo wa Ramadhani ulileta mabadiliko makubwa.

Barasi na Belgasem wamepongeza jitihada za mji na kujitolea kuhakikisha Waislamu wanapata msikitni.

Naye Farwell alisema anawashukuru vivyo hivyo, na pia amepongeza nia ya  Jumuiya ya Kiislamu ya Newfoundland kusaidia mji kufanya Gander kuwa mahali pazuri pa kuishi.

3480145

Kishikizo: waislamu canada msikiti
captcha