IQNA

Sura za Qur'ani Tukufu /26

Mantiki ya Mitume katika Sura Ash-Shu’ara

21:11 - August 19, 2022
Habari ID: 3475649
TEHRAN (IQNA) – Mwenyezi Mungu ametuma Mitume wengi kuwaongoza wanadamu na walikumbana na matatizo na masaibu mengi katika njia hii.

Kwa mfano, baadhi ya watu ambao walikuwa na dhambi na makosa, hawakukubali kwa urahisi kurekebisha njia yao. Haya hata hivyo hayangedhoofisha azma imara ya manabii na kudhoofisha mantiki yao.

Sura ya 26 ya Qur'ani Tukufu ni Sura Ash-Shu’ara. Ni Makki, ina Aya 227, na iko katika Juzuu ya 19 ya Kitabu kitukufu. Ni Sura ya 47 iliyoteremshwa kwa Mtukufu Mtume Muhammad (SAW).

Jina la Ash-Shu’ara (washairi) linatokana na kutajwa kwa washairi katika aya za 224 hadi 227 za Sura. Mistari hii inazungumza juu ya washairi ambao huandika mashairi yasiyo na maana na hawafungamani na maadili mema wala imani. Aya hizo pia zinawasifu washairi ambao ni waumini na ambao huwakumbusha watu kuhusu Mwenyezi Mungu. Kwa mtazamo huu, mashairi ni njia ya kutoa mwelekeo kwa jamii na inaweza kutumika katika njia ya imani na kujitolea.

Mfasiri maarufu wa Qur'ani Allamah Tabatabai anaamini kwamba lengo kuu la Sura Ash-Shu'ara ni kumpa ujasiri na kumtia moyo Mtukufu Mtume Muhammad (SAW) mbele ya waliokuwa wakimkana na uwekaji wao wa tuhuma dhidi yake. Allamah Tabatabai anasema kwamba Sura inasimulia hadithi za Mitume wa Mwenyezi Mungu waliotangulia na yale yaliyowapata maadui zao ili kuwaonya wale wanaoukanusha ujumbe wa Mtukufu Mtume Muhammad (SAW) wapate somo kutokana na yaliyowasibu waliotangulia.

Sura hii inazungumzia mienendo ya Mitume wa Mwenyezi Mungu, kutoka kwa Nuh hadi kwa Muhammad (SAW) na inasisitiza juu ya kanuni kama vile Tauhidi, Siku ya Kiyama, wito wa Mitume wa Mwenyezi Mungu, na umuhimu wa Qur'ani Tukufu.

Aidha sura hii inataja baadhi ya mazungumzo baina ya Mitume kama Ibrahim (AS), Nuhu (AS), Hud (AS), Salih (AS) na Lut (AS), na watu wao. La muhimu ni kwamba watu hao walipuuza yale waliyoambiwa na manabii na hivyo walikumbana na aina fulani ya adhabu kutoka kwa Mwenyezi Mungu.

Kwa mujibu wa fikra zilizotajwa katika Sura Ash-Shu’ara, inaweza kugawanywa katika sehemu tatu:

Sehemu ya kwanza inaangazia utukufu wa Qur'ani na inamtia moyo Mtukufu Mtume (SAW) mbele ya ukaidi na ukanushaji wa washirikina. Vile vile inaashiria dalili za Tuhidi na kufafanua sifa za Mwenyezi Mungu.

Sehemu ya pili inahusiana na hadithi za maisha ya manabii na mapambano yao, zikielekeza kwenye mantiki na hoja walizotumia kuwaongoza watu. Pia inazungumzia yaliyotokea kwa wakanushaji.

Sehemu ya tatu ni hitimisho la sehemu zilizotangulia na pia inajumuisha habari njema kwa waumini na mapendekezo kwa Mtukufu Mtume (SAW) kuhusu kuwalingania watu kwenye Uislamu na jinsi ya kuwatendea waumini.

Habari zinazohusiana
captcha