IQNA

Sura za Qur'ani Tukufu /44

Hatima ya wakanushaji wa ukweli kama ilivyotajwa katika Surah Ad-Dukhan

16:19 - December 03, 2022
Habari ID: 3476188
TEHRAN (IQNA) – Ukweli wa kila kitu uko wazi na dhahiri lakini wengine wanakanusha kwa sababu mbalimbali, kama vile kuepuka tishio kwa maslahi yao binafsi au ya kikundi.

Ndiyo maana wakandamizaji na madhalimu wengi katika historia walijaribu kuwakataa wajumbe wa Mwenyezi Mungu ili kuokoa utawala wao. Mwenyezi Mungu ameonya kutakuwa na adhabu kali na ya hakika kwao na hii imetajwa katika Sura kadhaa za Qur'ani Tukufu, ikiwa ni pamoja na Surah Ad-Dukhan.

Ad-Dukhan ni jina la Surah ya 44 ya Qur'ani Tukufu, ambayo ina aya 59 na iko katika Juz 25. Ni Sura ya Makki na sura ya 64 ya Qur'ani Tukufu iliyoteremshwa kwa Mtukufu Mtume Muhammad(SAW).

Jina lake linatokana na neno katika Aya ya 10. Aya hii inazungumzia adhabu iitwayo Dukhan kwa makafiri na moja ya alama za Siku ya Kiyama.

Dukhan inamaanisha kitu chenye gesi ambacho ni kama moshi na kitafunika anga yote kabla ya Siku ya Ufufuo.

Kwa mujibu wa Tafisiri ya Qur'ani Tukufu ya Al-Mizan, lengo kuu la Sura hii ni kuonya kuhusu adhabu katika dunia hii na ijayo kwa makafiri wanaokanusha ukweli wa Qur'ani.

Surah Ad-Dukhan pia inaashiria namna Qur'ani Tukufu iliyoteremshwa katika Usiku wa Qadr ili kuwaongoza wanadamu.

Inaanza kwa kusisitiza adhama ya Qur'ani Tukufu na ukweli kwamba iliteremka katika Usiku wa Qadr. Kisha inazungumzia Tauhidi na baadhi ya alama za adhama ya Mwenyezi Mungu duniani.

Kisha Sura inabainisha hatima ya makafiri na aina ya adhabu watakayoipata Siku ya Kiyama.

Halikadhalika inabainisha kwamba makafiri hivi karibuni watazungukwa na adhabu kali. Kisha watarejea kwa Muumba wao na Mwenyezi Mungu atayatathmini matendo yao na kuwapa adhabu ya milele.

Sura hii pia inaashiria kisa cha Nabii Musa (AS) na Bani Isra’il, makabiliano yao na Firauni na hatima yao.

Wakati Musa (AS) alipokwenda kwa Firauni kuwaokoa Bani Isra’il, Firauni na wafuasi wake walimkadhibisha na kwa hiyo, waliadhibiwa na Mungu na wakazama. Hadithi hii inalenga kuwaamsha wale wanaokataa ukweli.

Mbali na adhabu katika ulimwengu huu, Surah Ad-Dukhan inazungumza juu ya adhabu chungu zinazowangojea makafiri motoni. Inasisitiza kwamba hakika Siku ya Kiyama itakuja, watake wasitake. Kisha inaeleza yatakayotokea siku hiyo na aina za adhabu watakazozipata makafiri pamoja na baadhi ya malipo watakayopewa Waumini.

Makusudio ya uumbaji na ukweli kwamba mbingu na ardhi hazikuumbwa bure ni miongoni mwa mambo mengine yaliyotajwa katika Sura hii.

Jinsi ilivyoanza, Surah Ad-Dukhan inahitimisha kwa kusisitiza adhama ya  Qur'ani Tukufu.

Habari zinazohusiana
captcha