IQNA

Shakhsia katika Qur’ani /19

Yusuf; Nafasi ya kwanza katika simulizi nzuri zaidi ya Qur’ani Tukufu

22:35 - December 05, 2022
Habari ID: 3476202
TEHRAN (IQNA) – Nabii Yusuf ameelezewa kuwa ni mtume ambaye alikuwa na sura nzuri na mwenye utambuzi na ujuzi.

Kwa ujuzi wake wa kufasiri ndoto, aliweza kutabiri njaa huk Misri na kuisimamia kwa njia ambayo watu wangeweza kuvumilia miaka saba ya njaa bila matatizo makubwa.

Yusuf (AS) alikuwa miongoni mwa Mitume wa Bani Isra’il. Yaqub alikuwa baba yake na jina la mama yake lilikuwa Raheel. Alikuwa na kaka 11. Benyamini alikuwa ndugu yake kamili na wengine walikuwa ndugu wa kambo.

Qur'ani Tukufu inamuelezea Yusuf (AS) kuwa ni mmoja wa waja safi na wachamungu wa Mwenyezi Mungu. Jina lake limetajwa katika Qur’ani Tukufu mara 27 na Sura ya 12 imetajwa kwa jina lake.

Katika Surah Yusuf, hadithi ya maisha yake imewasilishwa kwa kina. Qur’ani Tukufu inaiita sura hii Ahsan al-Qasas (hadithi au simulizi bora zaidi). Inatoa maelezo kuhusu utoto wa Yusuf, jinsi ndugu zake walivyomtupa kisimani, jinsi alivyouzwa kuwa mtumwa wa mtawala wa Misri, kisa cha Zuleikha, jinsi Yusuf alivyotupwa jela, kukutana kwake na ndugu zake na baba yake, na jinsi alivyokuwa mtawala wa Misri.

Yusuf (AS), ambaye alikuwa na dalili za utume tangu akiwa mtoto, alipewa kipaumbele maalum na baba yake na hilo lilipelekea kijicho cha kaka yake.

Moja ya matukio makubwa katika maisha ya Yusuf lilikuwa ndoto aliyokuwa nayo. Aliota jua, mwezi na nyota kumi na moja zikiinama mbele yake. Baba yake, ambaye alijua tafsiri ya ndoto, alimsihi Yusuf asimwambie mtu yeyote kuhusu hilo kwa sababu liliashiria hadhi yake ya kuwa nabii na ikiwa wengine wangefahamu kuhusu hilo, hilo lingewatia wivu.

Wivu wa ndugu hao ulikuwa mkubwa kiasi kwamba walimtupa kwenye kisima na kumwambia Yaqub (AS) kwamba mbwa mwitu amemla.

Kundi la watu waliokuwa wakipita njiani walimuokoa Yusuf (AS) kutoka kisimani kisha wakamuuza kama mtumwa kwa mtawala wa Misri. Kisha Zuleikha, mke wa mtawala, akampenda Yusuf (AS) na baada ya kukataa kwake kujiunga naye katika uhusiano wa uzinzi, alimshutumu kwa kukosa uaminifu na akatupwa jela.

Baada ya miaka kadhaa, Yusuf (AS) alithibitisha kutokuwa na hatia na aliachiliwa kutoka gerezani. Kisha akawa maarufu kwa mtawala baada ya kutafsiri ndoto ya mtawala na kutoa mipango ya kutatua suala la njaa nchini Misri.

Alisimamia jitihada za kukabiliana na njaa kwa njia ambayo Misri na nchi jirani hazikukabili matatizo yoyote makubwa wakati wa miaka saba ya njaa.

Wakati Yusuf (AS) alipofikisha miaka 120, Mwenyezi Mungu alimuamuru kukabidhi nuru na Hikma aliyokuwa nayo kwa Babraz ibn Lawi bin Yaqub.

Alimwita Babraz na watoto wengine na wajukuu wa Yaqub (AS), ambao walikuwa karibu wanaume 80 wakati huo, na kuwaambia kwamba kikundi kitawashinda hivi karibuni na kuwakandaiza kabla ya Mwenyezi Mungu kuwaokoa kupitia mmoja wa wana wa Lawi aitwaye Musa (AS).

Baada ya Yusuf (AS) kufariki, kila kundi la watu lilitaka kumzika katika mtaa wao. Ili kuzuia mapigano, walimweka kwenye sanduku la marumaru na kumzika kwenye Mto Nile. Miaka kadhaa baadaye, Nabii Musa (AS) aliutoa mwili wake hapo na kumzika huko Palestina.

captcha