IQNA

Maandamano ya Wamorocco kupinga uhusiano na Israel

18:00 - December 06, 2022
Habari ID: 3476209
TEHRAN (IQNA) - Watu wamefanya maandamano katika maeneo tofauti ya Morocco ili kutoa maoni yao ya kupinga kuhalalisha uhusiano na utawala wa Kizayuni wa Israel.

Washiriki wa maandamano hayo yaliyoandaliwa katika miji tofauti kama vile mji mkuu Rabat, walibeba bendera za Palestina na kupiga nara dhidi ya uhusiano wa karibu na utawala wa Tel Aviv.

Walitoa wito kwa watawala wa Morocco kufikiria upya kuanzisha uhusiano na utawala dhalimu wa Israel unaokalia ardhi za Palestina kwa mabavu.

Maandamano hayo yanakuja wakati serikali ya Morocco inaandaa mkutano unaoitwa "Elimu na Kuishi pamoja", unaohudhuriwa na maafisa wa utawala haramu wa Israel.

Nchi nyingine kadhaa za Kiarabu, zikiwemo Bahrain, Jordan na Umoja wa Falme za Kiarabu, pia zinahudhuria mkutano huo unaojulikana kwa jina la N7.

Mkutano huo wa siku tatu, ulioratibiwa kwa pamoja na Baraza la Atlantiki na Wakfu wa Jeffrey M. Talpins, unafanyika Rabat.

Wakati nchi za Kiarabu ambazo zimeweka uhusiano wa kawaida na Israel hazijapata maendeleo katika eneo lolote, hata katika uchumi, katika kipindi cha miaka miwili iliyopita, wazungumzaji katika mkutano huo walipongeza kile walichokiita maendeleo katika ushirikiano kati ya Israel na Waarabu tangu kusainiwa kwa mikataba ya kuhalalisha.

Serikali ya Morocco ilianzisha uhusiano wa kidiplomasia na utawala wa Israel mwezi Disemba 2020, kufuatia hatua kama hiyo ya UAE, Bahrain na Sudan.

Waislamu duniani kote, ikiwa ni pamoja na katika nchi hizi nne, wamelaani hatua hiyo na kusema ni usaliti wa kadhia ya Palestina.

 4104868

Kishikizo: morocco israel palestina
captcha