IQNA

Umoja wa Waislamu

Ujumbe wa Rais wa Iran kwa kongamano la kimataifa la nchi za Kiislamu nchini Russia

22:03 - December 09, 2022
Habari ID: 3476223
TEHRAN (IQNA)- Kongamano la 18 la kimataifa linalofanyika kwa anuani ya "Uislamu, Uadilifu na Mlingano, Misingi ya Dini na Nidhamu ya Ulimwengu" umeanza rasmi katika mji mkuu wa Russia, Moscow na kufunguliwa kwa salamu za Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

 Zaidi ya shakhsia 150 wakiwemo maulamaa, mashekhe na wanafikra Waislamu wa madhehebu za Sunni na Shia kutoka nchi 40 za Kiislamu wanahudhuria mkutano huo unaofanyika kwa mnasaba wa kuadhimisha mwaka wa elfu moja na moja tangu Uislamu ulipoingia katika ardhi ya Urusi.

Katika hafla ya ufunguzi, Hujjatul-Islam Abulqasem Dolabi, mshauri wa Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, almesoma ujumbe wa salamu za Rais Seyyed Ebrahim Raisi kwa washiriki wa mkutano huo wa kimataifa.

Katika salamu zake hizo, Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema: "dini ya Uislamu ilidhihiri katika kipindi cha historia ya ulimwengu huu wakati giza totoro la dhulma, ujahili, uonevu, ufisadi na upotofu lilikuwa limegubika maisha ya jamii ya wanadamu; na hapo ndipo Mtume SAW, ambaye ni ruwaza na kigezo cha umaanawi na akhlaqi njema, alipowaletea wanadamu hidaya ya suluhu na amani kupitia nuru ya uadilifu na kuwaonyesha njia ya saada na uongofu".

Katika sehemu nyingine ya salamu na ujumbe wake huo, Sayyid Ebrahim Raisi amesema: "kama inavyothibitishwa na historia, Russia ni moja ya sehemu za kwanza kufika Uislamu katika nchi za mbali; na Wairani Waislamu wanajivunia kwamba mji wa kihistoria wa Darband, ambao ni kitovu cha muunganisho na makutano ya utamaduni wa Urusi, Iran na Uislamu ni njia na kituo kikuu walipofikia Waislamu katika ardhi hiyo pana ya Urusi.

Mkutano huo wa siku mbili ulioanza jana, unashirikisha pia wawakilishi kutoka Idara ya Mufti wa Russia, Jumuiya ya Al-Mustafa Al-Alamiya ya Iran, Shirika la Masuala ya Dini la Uturuki na jumuiya za kidini za Waislamu wa Kisuni na Kishia wa Russia, ambapo wawakilishi wa nchi washiriki watawasilisha na kubainisha fikra na mitazamo yao juu ya namna ya kuimarisha umoja, uadilifu, amani na udugu baina ya Waislamu.

4105672

captcha