IQNA

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu

Maadhimisho 22 Bahman mwaka huu yatakuwa dhihirisho la umoja wa kitaifa na kusambaratisha stratijia ya adui

20:13 - February 08, 2023
Habari ID: 3476530
TEHRAN (IQNA)- Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amekutana na mamia ya makamanda na wafanyakazi wa Kikosi cha Anga na Ulinzi wa Anga cha Jeshi la Iran na kusema: "Bahman 22 (11 Februari) mwaka huu itakuwa madhihirisho ya umoja wa kitaifa," na kuongeza kuwa, "Bahman 22 mwaka huu itakuwa ni dhihirisho la izza na kuaminiana wananchi pamoja na umoja wa kitaifa."

Kwa mujibu wa tovuti ya Ofisi ya Kiongozi Muadhamu, Ayatulah Khamenei katika mkutano  huo wa leo mjini Tehran amesisitiza kuwa: "Siku ya 22 Bahman kama ambavyo imebakia hai hadi sasa inapaswa kubakishwa hai pia katika mustakabali na kuongeza kuwa, mapinduzi hai ni mapinduzi ambayo yanabakisha hai madhihirisho yake na katika kila zama, kwa kutambua mahitajio na hatari zilizopita, yanakidhi mahitajio yaliyopo na kusambaratisha hatari zinazoibuka." 

22 Bahman au Februari 11 ni siku ya kuadhimisha ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran ya mwaka 1979.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema sababu ya kushindwa au kurejea udikteta sugu na wenye machungu katika mapinduzi makubwa ya dunia kama vile mapinduzi ya Ufaransa na Shirikisho la Sovieti ni kughafilika kutokana na mahitajio na hatari zilizopo sambamba na kujishughulisha na masuala ya malumbano ya watu binafsi na kuongeza kuwa, Mapinduzi ya Kiislamu yameweza kujikinga na dosari hizi.

Ayatullah Khamenei ameendelea kubaini kuwa, malengo ya wazi ya maadui dhidi ya mfumo wa Kiislamu ni kuyapigisha magoti Mapinduzi ya Kiislamu na kuongeza kuwa Mapinduzi ya Kiislamu yameweza kuwaondoa maadui kutoka katika eneo hili muhimu, la kimkakati na lenye utajiri. Aidha amesema Mapinduzi ya Kiislamu yameweza kupaza sauti ya uhuru na kutosalimu amri na nukta hizi si tu kuwa ni za kisiasa bali zimegeuka na kuwa imani na itikadi za kidini.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amefafanua kuwa, yamkini baadhi ya nchi zinataka kuwa na sera huru zisizotegemea Marekani lakini sera hizo hubadilika kutokana na masuala ya kisiasa, mazungumzo, kukaa kwenye meza ya mazungumzo na hata kuhongwa baadhi ya watu wenye ushawishi, na mifano ya hayo inaonekana sehemu nyingi duniani.

Ayatullah Khamenei aidha amesema leo Jeshi la Iran ni nembo ya uhuru na kujitegemea, uimara na pia ni jeshi ambalo ni azizi miongoni mwa wananchi na maafisa wa Iran. Ameendelea kusema kuwa, leo Jeshi liko na wananchi na wananchi wako pamoja na jeshi. Aidha amesema huko kabla ya mapinduzi wanajeshi walikuwa hawana haki hata ya kugusa vipuri vya ndege vilivyonunuliwa kutoka Marekani lakini leo pamoja na kuwepo vikwazo jeshi limeweza kujiundia ndege na kutekeleza miradi mingine mikubwa ambayo imewaletea wananchi heshima na mfano wa hilo ni uzinduzi uliofanyika jana.

Kiongozi Muadhamu hapo alikuwa akiashiria hatua ya Jeshi la Anga la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ya kuzindua  kituo cha ndege kilicho chini ya ardhi ambacho kimepewa jina la "Oqab 44" (Tai 44). Kituo hicho cha siri kina aina mbalimbali za ndege za kivita na mabomu pamoja na ndege zisizo na rubani au droni za Jeshi la Anga.

Wakati huo huo, katika kikao hicho cha leo Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ametuma salamu za rambi rambi kufuatia mitetemeko mikubwa ya ardhi nchini Uturuki na Syria  na kusema: "Tumesikitishwa na msiba uliowakumba ndugu zetu nchini Syria na Uturuki. Tunamuomba Mwenyezi Mungu awarehemu waliopoteza maisha na pia awape subira na utulivu wa kiroho waliokumbwa na msiba. Sisi wenyewe tumewahi kukumbwa na yaliowakuba na hivyo tunadiriki hali inavyokuwa ya majonzi wakati zilzala inapojiri na familia kupoteza maisha. Iran imetuma misaada na itaendelea kutuma misaada."

4120659

captcha