IQNA

Harakati za Qur'ani

Rais wa Maldives ahimiza kutafuta nguvu katika Qur’ani Tukufu wakati wa Mwezi wa Ramadhani

18:13 - March 21, 2023
Habari ID: 3476738
TEHRAN (IQNA) - Rais wa Maldives (Maldivi) alitoa wito kwa watu kuutumia vyema mwezi mtukufu wa Ramadhani, ambao huenda ukaanza siku ya Alhamisi, na kutafuta faraja na nguvu katika mwanga wa nuru ambayo ni Qur’ani Tukufu.

Akizungumza katika hafla ya kufunga Mashindano ya 35 ya Kitaifa ya Kuhifadhi Qur'ani ya Maldives, Ibrahim Mohamed Solih amewataka wananchi siku ya Jumatatu kuutumia vyema mfungo wa mwezi wa Ramadhani, kutafuta faraja na nguvu katika mwanga wa Qur'ani Tukufu, na kubaki imara katika njia ya mafundisho ya kidini na tabia njema.

Katika hafla hiyo katika Kituo cha Kiislamu, Solih aliwapongeza washindi na kueleza umuhimu wa kuhifadhi na kutekeleza sheria za Tajwid za Qur'ani Tukufu kwa sasa na akhera.

Solih pia aliashiria idadi kubwa ya waliohifadhi Qur’ani Tukufu  nchini Maldives na akazungumzia umuhimu wa kuchukuliwa hatua zaidi kudumisha heshima yao. Vile vile amewataka wananchi kuhoji sababu za kuwaalika waliohifadhi Qur’ani Tukufu kutoka nchi nyingine kuongoza swala ya Tarawih katika mwezi wa Ramadhani.

Akisisitiza  tena dhamira ya utawala katika kudumisha na kulinda  maadili na kanuni za Uislamu na Qur'ani Tukufu, amewataka wote kujitahidi kwa bidii katika kuwafundisha watoto wadogo.

Aidha Solih alitoa wito kwa taasisi za elimu ya juu kuendeleza mafundisho ya Qur'ani Tukufu na ujumbe wa Uislamu, unaoungwa mkono na utafiti wa kisayansi na maendeleo ya kiteknolojia katika ulimwengu wa kisasa.

Katika sherehe hizo, rais wa Maldives alitoa tuzo za juu zaidi katika kategoria za qiraa na kuhifadhi, pamoja na tuzo za juu za taasisi inayoongoza na washindi wakuu wa shindano.

Maldives au Maldivi ni nchi huru kwenye funguvisiwa la Maldivi katika Bahari Hindi katika eneo la kusini mwa Asia. Nchi hiyo inajumuisha  visiwa 1,192 na kati ya hivyo takriban 200 hukaliwa na watu. Idadi ya watu katika nchi hiyo ndogo inakadiriwa kuwa nusu milioni na asilimia 100 ya raia wa nchi hiyo ni Waislamu.

3482878

Kishikizo: qurani tukufu maldives
captcha