IQNA

Mwezi wa Ramadhani

Nchi nyingi za Kiislamu zatangaza Alhamisi kuwa Siku ya Kwanza ya Ramadhani

10:22 - March 22, 2023
Habari ID: 3476741
TEHRAN (IQNA) – Nchi nyingi za Kiislamu katika eneo la Asia Magharibu au Mashariki ya Kati zimetangaza Alhamisi, Machi 23, kuwa mwanzo wa mwezi mtukufu wa Ramadhani.

Katika Jamhuri ya Kiislamu ya Iran  Kamati ya Istihlal (kuutafuta mwezi mwandamo) ya Ofisi ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu imetangaza kwa Alhamisi ya kesho  23 Machi itakuwa siku ya kwanza ya Mwezi Mtukufu wa Ramadhani.

Jana Idara ya Mahakama  Saudi Arabia ilitangaza kwamba kwa sababu mwezi haukuonekana Jumanne jioni na kwa msingi huo leo Jumatano ndiyo siku ya mwisho ya mwezi wa Shaban na Ramadhani Alhamisi.

Kamati ya Istihlal  nchini Qatar pia iimebaini kuwa Alhamisi ni siku ya kwanza ya Ramadhani, Al Jazeera iliripoti.

Halikadhalika wahusika nchini Kuwait na Umoja wa Falme za Kiarabu pia walitangaza kwamba mwezi mwezi mwandamo haukuonekana Jumanne jioni na, kwa hiyo, Jumatano ndiyo siku ya mwisho ya Shaaban.

Kwa mujibu wa Idara ya Awqaf ya Kisunni ya Iraq pia, Alhamisi itaashiria mwanzo wa mwezi wa mfungo. Halikadhalikak Ofisi ya Ayatullah Sistani, Marjaa Taqlid wa Mashia Iraq nayo imetangaza katika taarifa kuwa Alhamisi itakuwa siku ya kwanza ya Ramadhani.

Shirika rasmi la habari la Syria SANA limenukuu Baraza la Fiqh la Wizara ya Awqaf ya nchi hiyo ya Kiarabu ikitangaza Alhamisi itakuwa siku ya kwanza ya Ramadhani.

Lebanon, Sudan na Misri ni miongoni mwa nchi nyingine za Kiislamu katika Mashariki ya Kati ambako Waislamu wataanza kufunga siku ya Alhamisi.

Ramadhani ni mwezi wa tisa wa kalenda ya Kiislamu na ni kipindi cha  ambacho Waislamu duniani kote hujizuia kula na kunywa mchana na pia hujuzuia na mambo mengine yote ambayo yamekatazwa katika mwezi huu huku wakikithirisha Uchamungu, ibada, na utoaji wa sadaka.

Qur'ani Tukufu iliteremshiwa Mtume Muhammad SAW katika mwezi huu mtukufu wa Ramadhani na Waislamu hutumia muda mwingi katika mwezi huu kuisoma Qur'ani Tukufu na kutafakari kuhusu aya zake.

Waislamu kote ulimwenguni wana salamu mbali mbali za Mwezi wa Ramadhani katika lugha zao za asili ambapo “Ramadan Mubarak” na “Ramadan Kareem” ni salamu za kawaida zinazotumiwa na wote katika kipindi hiki, kwa ajili ya kumtakia muumini  mwezi wenye baraka na ukarimu.

Mwishoni mwa Ramadhani, Waislamu husherehekea siku kuu ya Idul Fitr kwa kujumuika katika Sala ya Jamaa asubuhi.

4129384

Habari zinazohusiana
captcha