IQNA – Kozi maalum ya maandalizi ya waamuzi wa mashindano ya Qur’ani nchini Iraq imefikia tamati kwa hafla adhimu.
Kituo cha Kitaifa cha Sayansi ya Qur’ani, kilicho chini ya usimamizi wa Idara ya Awqaf ya Kishia nchini Iraq, kilihitimisha kozi yake maalum ya mafunzo kwa waamuzi wa mashindano ya ndani ya Qur’ani siku ya Jumatatu jioni, kupitia sherehe iliyofanyika katika Msikiti wa Imam Ali (AS).
Hafla hiyo ilihudhuriwa na Qari Rafi Al-Amiri, Mkurugenzi wa kituo hicho, pamoja na idadi ya viongozi wa Qur’ani na wanazuoni wa kidini.
Sherehe ilianza kwa usomaji wa aya za Qur’ani Tukufu na Qari Farhan Al-Arqawizi, ikifuatiwa na hotuba iliyotolewa na Dkt. Al-Amiri.
Katika hotuba yake, Dkt. Al-Amiri alisisitiza umuhimu wa kozi hiyo, iliyoanza mwezi Mei, na umuhimu wa kuweka msingi thabiti wa kuandaa mashindano ya Qur’ani yenye waamuzi waliohitimu vyema.
Pia alitoa shukrani za dhati kwa juhudi za jopo la walimu wa kituo hicho na mchango wao katika kufanikisha kozi hii maalum ya Qur’ani, na kuwapongeza washiriki kwa kujitolea kwao katika kukuza ujuzi wa kuhukumu kwa kutumia mbinu na miongozo ya kisasa zaidi ya mashindano ya Qur’ani.
Mwishoni mwa hotuba yake, alitoa shukrani kwa uongozi wa Msikiti wa Imam Ali (AS) kwa ushirikiano wao na Kituo cha Kitaifa cha Sayansi ya Qur’ani katika kuandaa kozi hii.
Baadaye, Sheikh Ahmad Al-Sarai, Mkurugenzi wa Msikiti wa Imam Ali (AS), aliwapongeza washiriki kwa kuhitimisha kwa mafanikio kozi hiyo, na kumshukuru Mkurugenzi wa kituo hicho pamoja na wakufunzi kwa juhudi zao za kutukuka katika kueneza utamaduni wa Qur’ani na kukuza uwezo wa walimu wa Qur’ani.
3498701