IQNA

13:07 - August 19, 2026
Habari ID: 3482648

Misikiti ya kihistoria ya Kosovo ni hazina ya kumbukumbu ya kitaifa

IQNA – Misikiti ya kihistoria nchini Kosovo inapaswa kutazamwa kama sehemu ya msingi ya urithi wa kiutamaduni na kihistoria wa taifa hilo, si kama maeneo ya ibada pekee, afisa mmoja wa Jumuiya ya Kiislamu amesema.

k

Ramadan Shkodra, Mkuu wa Idara ya Uchapishaji na Utamaduni katika Urais wa Jumuiya ya Kiislamu ya Kosovo, alitoa kauli hiyo katika makala mpya ya uchambuzi, akisisitiza nafasi ya urithi wa Kiislamu katika uundaji wa kumbukumbu ya taifa.

Katika makala yake, Shkodra anaeleza kuwa misikiti ya Kosovo ni ushahidi thabiti wa maendeleo ya kijamii, kimajengo na kiutamaduni ya nchi hiyo. Anaonyesha kuwa historia ya misikiti hiyo imefungamana kwa karibu na taasisi ya wakfu (waqf), ambayo kwa karne nyingi imekuwa nguzo ya kusaidia taasisi za kidini, elimu, huduma za jamii na manufaa ya umma.

Kwa mujibu wake, urithi wa kiutamaduni wa Kosovo umejengwa kupitia mwingiliano wa ustaarabu, tamaduni na mila mbalimbali, huku urithi wa Kiislamu ukiwakilisha tabaka muhimu la kihistoria lililokua kwa zaidi ya karne tano. Anaandika kuwa misikiti ina umuhimu maalum kwa sababu huunganisha usanifu, sanaa na historia, na huakisi kwa pamoja mapokeo ya Kiislamu na ustadi wa kienyeji wa Kialbania.

Shkodra anaongeza kuwa misikiti mingi ilijengwa au kuungwa mkono na wafadhili, wakuu na wahisani wa Kialbania, jambo linaloifanya iwe ushahidi si tu wa maisha ya kidini, bali pia wa utamaduni wa muda mrefu wa kutoa wakfu na hisani katika jamii ya Kialbania. Kwa mtazamo wake, jukumu la misikiti kihistoria halikuishia katika ibada pekee; bali pia iliwa vituo vya elimu, maisha ya kijamii na maendeleo ya miji, utamaduni na uchumi.

Mwandishi huyo pia anajadili alichokiita kuwekwa pembezoni kwa urithi wa Kiislamu katika vipindi fulani vya historia ya kisasa ya Kosovo. Anaeleza kuwa baadhi ya simulizi zenye athari za historiografia ya Serbia zilijaribu kuonyesha alama za Kiislamu kama vitu vya kigeni au vilivyowekwa kwa kulazimishwa, badala ya kuzitambua kama sehemu ya historia halisi ya Kosovo.

Aidha, anaandika kuwa katika kipindi cha ujamaa cha Yugoslavia ya zamani, misikiti kadhaa na taasisi nyingine za Kiislamu ziliharibiwa au kubomolewa, mara nyingine kwa kisingizio cha usasa wa miji au sera za serikali. Kwa mujibu wake, uharibifu wa urithi wa Kiislamu ulifikia kiwango kikubwa zaidi wakati wa Vita vya Kosovo mwaka 1998 na 1999, ambapo misikiti 218 ilishambuliwa, kuharibiwa au kubomolewa, huku madrasa, tekke, mali za wakfu, maktaba na hifadhi za kihistoria pia zikilengwa.

Shkodra anaueleza uharibifu huo kuwa haukuwa dhidi ya majengo ya ibada pekee, bali pia dhidi ya kumbukumbu ya kihistoria na kiutamaduni ya Waalbania wa Kosovo. Anasema kupotea kwa alama hizo kulipunguza utajiri wa jumla wa urithi wa Kosovo.

Pia anatoa wito wa kuongezwa kwa uhakiki wa kitaaluma, ukarabati wa kitaalamu na utambuzi wa kitaasisi wa urithi wa Kiislamu wa nchi hiyo. Anaashiria juhudi za hivi karibuni za Wizara ya Utamaduni ya Kosovo za kurejesha na kuhifadhi baadhi ya misikiti yenye thamani kubwa ya akiolojia na usanifu kama hatua chanya.

Anataja maonyesho ya “Kumbukumbu Katika Picha – Misikiti Iliyoharibiwa Bosnia na Herzegovina na Kosovo Katika Miaka ya 1990: Mauaji ya Kimbari ya Kidini Yaliyopangwa"  yaliyofanyika Pristina tarehe 18 Desemba 2025, kama mfano wa juhudi za kuhifadhi kumbukumbu ya urithi wa kidini uliodhulumiwa. Anaongeza kuwa makala zilizowasilishwa katika ufunguzi wa maonyesho hayo zilichapishwa baadaye katika Edukata islame, zikihamisha maudhui hayo kutoka maonyesho ya picha hadi katika kazi ya kitaaluma na ya nyaraka.

Kwa Shkodra, kulinda misikiti ya kihistoria pia ni kulinda historia ya mfumo wa wakfu ulioisaidia kujengwa na kusimama. Anaamini kuwa kuhifadhi urithi huu kunahitaji kulinda si majengo pekee, bali pia nyaraka zake, simulizi zake, kazi zake na uhusiano wake na jamii zilizoiunda na kuitumia.

Kwa jumla, anahitimisha kuwa kurejesha hadhi ya kihistoria ya misikiti ya Kosovo na wakfu zake za Kiislamu hakumaanishi kurudi tu kwenye historia, bali ni juhudi ya kuhuisha sehemu muhimu ya kumbukumbu ya kiutamaduni ya taifa hilo na kuiingiza katika uelewa wa kisasa wa historia na utambulisho wake.

3498704

Kishikizo: kosovo msikiti waislamu
captcha