IQNA – Polisi wamewakamata watu kadhaa katika mji wa Dearborn, jimbo la Michigan nchini Marekani, baada ya maandamano dhidi ya Uislamu kuwaleta pamoja mamia ya waandamanaji wa kupinga maandamano hayo na kusababisha kuimarishwa kwa ulinzi.
Mtu anayejulikana kwa vitendo vya chuki dhidi ya Uislamu na kuvunjia heshima Qur’ani Tukufu, Jake Lang, pamoja na wafuasi wake, walikusanyika Jumanne nje ya Maktaba ya Henry Ford Centennial kwa ajili ya hafla aliyoiita “mkusanyiko wa Wapiganaji wa Kikristo” (Christian Crusader). Mvutano na makabiliano yalizuka kati yao na waandamanaji waliokuja kupinga tukio hilo.
Polisi wa Dearborn walithibitisha kuwa watu kadhaa wamekamatwa, lakini wakasema idadi kamili itatangazwa baadaye.
Mamlaka zilituma vikosi vya ziada vya usalama kabla ya maandamano hayo kufanyika.
Meya wa Dearborn, Abdullah Hammoud, alieleza athari za maandamano hayo kwa jamii ya Waislamu ya mji huo. Alisimulia jinsi alivyokutana na mtoto wa takribani miaka sita au saba aliyemuuliza iwapo waandamanaji walikuwa wanakuja kumuua.
“Watoto wetu wanasikiliza,” Hammoud alisema.
“Wanasikia mazungumzo yetu, wanaona vichwa vya habari, na wanaona wazazi wao wanapokuwa na wasiwasi.”
Baada ya siku kadhaa za kuongezeka kwa mvutano, Mwanasheria Mkuu wa Michigan, Dana Nessel, alithibitisha kuwa idara yake ilikuwa ikishirikiana moja kwa moja na Meya Hammoud, uongozi wa jiji pamoja na Idara ya Polisi ya Dearborn. Amesema kuwa rasilimali zote za jimbo zilitolewa na kwamba kulikuwa na ufuatiliaji wa pamoja kwa ajili ya kudumisha usalama wa umma.
Tukio hilo ni la hivi karibuni katika mfululizo wa uchochezi wa makusudi dhidi ya Waislamu unaodaiwa kufanywa na Lang mjini Dearborn, pamoja na vurugu zilizotokea wakati wa msafara wa kila mwaka wa Mazuwar wa Arbaeen mapema mwezi huu.
Lang, ambaye alishiriki katika ghasia za Januari 6 na baadaye akasamehewa, amekuwa akiandaa mara kwa mara maandamano dhidi ya Uislamu mjini Dearborn na amekufuru Qur’ani Tukufu mara kadhaa.
Tukio hilo limezua wasiwasi mkubwa miongoni mwa familia za Kiislamu, hasa kutokana na athari za kisaikolojia zinazowapata watoto na vijana wanaoshuhudia kauli za chuki, vitisho na vitendo vya kuchochea uhasama dhidi ya dini yao.
Kwa mujibu wa viongozi wa jamii, kulinda amani katika Dearborn kunahitaji si tu uwepo wa polisi, bali pia uwajibikaji wa kisheria dhidi ya vitendo vinavyolenga kuchochea chuki za kidini, kuvuruga utulivu wa jamii na kutishia usalama wa waumini. Habari hiyo pia inaangazia umuhimu wa mamlaka za Marekani kuchukua hatua madhubuti dhidi ya vitendo vya kuchafua vitabu vitakatifu na uchochezi unaolenga jamii za wachache.
3498705