IQNA

19:08 - August 20, 2026
Habari ID: 3482652

Rekodi yavunjwa ya waliojisajili Tuzo ya Kimataifa ya Qur’ani Tukufu ya Dubai

IQNA – Jumla ya maombi 20,500 kutoka nchi 135 yamewasilishwa kwa ajili ya toleo la 29 la Tuzo ya Kimataifa ya Qur’ani Tukufu ya Dubai (DIHQA).

T

Hii ndiyo idadi kubwa zaidi ya washiriki wa kimataifa katika historia ya tuzo hiyo.

Idadi hiyo kubwa imepatikana baada ya usajili kufungwa kwa toleo la mwaka 1448 Hijria–2027, linalofanyika chini ya udhamini wa Sheikh Mohammed bin Rashid Al Maktoum, Makamu wa Rais na Waziri Mkuu wa Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE), ambaye pia ni Mtawala wa Dubai.

Ongezeko hilo limefuatia mabadiliko yaliyoanzishwa chini ya dira ya maendeleo ya tuzo hiyo, “Katika Kutafuta Kisomo Kizuri Zaidi cha Qur’ani Duniani,” ikiwemo kuruhusu watu binafsi kutuma maombi moja kwa moja, sambamba na utaratibu wa jadi wa uteuzi kupitia nchi zao au vituo vya Kiislamu vilivyoidhinishwa.

Tuzo hiyo pia imeanzisha mfuko wa zawadi unaozidi dirham milioni 12 (dola milioni 3.3), ambao ni mkubwa zaidi katika historia yake, pamoja na mabadiliko katika makundi ya mashindano, vigezo vya kustahiki, mchakato wa tathmini na taratibu za ushiriki.

Misri imeongoza kwa idadi ya maombi, ikiwa na 6,838, ikifuatiwa na Indonesia yenye 1,923, Pakistan 1,862 na Syria 1,511.

Kundi la washindani wa kiume wenye umri wa zaidi ya miaka 16 lilipokea maombi 14,040, huku kundi la wavulana na wasichana walio chini ya miaka 16 likipokea maombi 6,495, yakiwemo 2,394 kutoka kwa washiriki wa kike.

Ahmed Darwish Al Muhairi, Mkurugenzi Mkuu wa Idara ya Masuala ya Kiislamu na Shughuli za Kichamii za Dubai na Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini ya Tuzo ya Kimataifa ya Qur’ani Tukufu ya Dubai, alisema ushiriki huo ambao umevunja rekodi unaonyesha athari ya mfumo mpya wa tuzo hiyo na kuongezeka kwa wigo wake kimataifa.

Chini ya mfumo mpya wa zawadi, mshindi wa nafasi ya kwanza katika kila moja ya makundi mawili makuu atapokea dola milioni 1. Washindi wa nafasi ya pili watapokea dola 100,000, huku washindi wa nafasi ya tatu wakipokea dola 50,000. Tuzo ya Mtu Binafsi wa Kimataifa wa Qur’ani nayo ina zawadi ya dola milioni 1.

Kipengele kingine kipya katika toleo la 29 ni kuwa washindani waliofuzu hatua ya mwisho wataalikwa Dubai wakati wa mwezi mtukufu wa Ramadhani ili kuongoza Swala za Tarawehe katika misikiti mikubwa. Baadaye, kura za umma zitatumika kumchagua “Msomaji Mzuri Zaidi wa Qur’ani Duniani.”

Kwa sasa, waombaji wanafanyiwa tathmini ya awali kwa kuzingatia kanuni za Tajwidi, ubora wa sauti, usomaji wa Qur’ani na utendaji wao kwa ujumla.

Kwa washindani wenye umri wa zaidi ya miaka 16, wale watakaofaulu hatua ya kwanza wataingia katika hatua ya upigaji kura wa umma, huku washindani waliochaguliwa katika hatua ya mwisho wakialikwa Dubai wakati wa Ramadhani. Upigaji kura umepangwa kufanyika kuanzia Februari 8 hadi 16, 2027.

Kwa washindani walio chini ya miaka 16, hatua ya pili itafanywa kupitia tathmini ya moja kwa moja kwa njia ya video kuanzia Septemba 1 hadi 14, 2026. Washindani watakaofuzu hatua ya mwisho wataingia katika hatua ya upigaji kura wa umma kuanzia Februari 8 hadi 16, 2027.

Tangu kuanzishwa kwake, jumla ya washindani 7,826 kutoka nchi 123 wameshiriki katika matoleo 28 ya mashindano hayo ya Qur’ani. Tuzo hiyo imetoa zaidi ya dirham milioni 67 kama zawadi tangu toleo lake la kwanza, na imetunuku watu 24 pamoja na taasisi tatu Tuzo ya Mtu Binafsi wa Kimataifa wa Qur’ani.

Habari zinazohusiana
captcha