IQNA

17:17 - August 22, 2026
Habari ID: 3482661

Programu za kuhifadhi Qur’ani kwa wanafunzi zahitimishwa nchini Jordan

IQNA – Programu za bure za kuhifadhi, kusoma, na kusahihisha usomaji wa Qur’ani (Tajweed) kwa wanafunzi wa shule nchini Jordan zimefikia tamati katika hafla maalum iliyofanyika siku ya Alhamisi.

Mohammad Khalaileh

Waziri wa Wakfu na Masuala ya Kiislamu wa Jordan, Mohammad Khalaileh, aliongoza hafla hiyo ya kuhitimisha programu hizo zilizowahusisha wanafunzi wa rika zote wakati wa likizo ya kiangazi.

Wizara ilizindua programu hizo mnamo mwishoni mwa mwezi Juni, kwa ushirikiano na Wizara ya Mazingira, ikiwa na kaulimbiu: “Mazingira Safi Zaidi… Jamii Iliyoelimika Zaidi.”

Programu hizi zilijumuisha shughuli mbalimbali za kielimu zinazolenga kuimarisha maadili ya kidini na utaifa miongoni mwa wanafunzi, pamoja na kutekeleza mipango ya kujitolea na kampeni za kuhimiza usafi na uelewa wa mazingira.

Katika hafla iliyohudhuriwa na Waziri wa Mazingira, Ayman Suleiman, Waziri Khalaileh alibainisha kuwa zaidi ya vituo 2,000 vinavyosimamiwa na Wizara ya Wakfu vinaendelea kufanya kazi mwaka mzima ili kuwafuatilia wanafunzi na kuimarisha mafanikio yaliyopatikana katika programu za kiangazi.

Akizungumza katika hafla hiyo, Khalaileh alisisitiza kuwa usafi si jukumu la wizara au manispaa pekee, bali ni jukumu la pamoja na utamaduni wa kijamii unaoambatana na mafundisho ya Uislamu na mwamko wa kibinadamu.

Hatem Suhaimat, Mkurugenzi wa Elimu ya Dini katika Wizara hiyo, alieleza kuwa takriban wanafunzi 211,000 wa kiume na wa kike walishiriki katika mwaka huu.

Kwa upande wake, Lamis Hazim, Mkurugenzi wa Masuala ya Wanawake katika Wizara hiyo, alisema kuwa jumla ya vituo 2,107 vya kiangazi vilitengwa kwa ajili ya wanawake, ambapo takriban wanafunzi 125,000 wa kike walijiunga.

Katika kuhitimisha hafla hiyo iliyohudhuriwa na maafisa wakuu wa wizara, Waziri Khalaileh aliwatunuku vyeti vituo 12 bora vya kiangazi, ikiwa ni kutambua juhudi zao na ufanisi wao katika kutekeleza programu na shughuli zilizopangwa wakati wa msimu huo.

3498725

Kishikizo: jordan qurani tukufu
captcha