IQNA – Taasisi ya Dar al-Ifta (Idara ya Fatwa) ya nchini Misri imesisitiza kuwa sherehe za maadhimisho ya kuzaliwa kwa Mtume Mtukufu Muhammad (SAW), maarufu kama Maulidi, ni utamaduni uliokita mizizi nchini humo.
Katika taarifa yake kupitia mtandao wa Facebook, Dar al-Ifta imesema kuwa kusherehekea kuzaliwa kwa Mtume Muhammad (SAW) kunamaanisha kudhihirisha furaha katika siku hii kwa kukusanyika ili kumkumbuka, kumsifu, na kumtukuza Mtume wa mwisho wa Mwenyezi Mungu, pamoja na kutoa chakula, kufunga sawm, na kuswali; yote haya yakifanyika kama ishara ya upendo kwa Mtume Muhammad (SAW).
Taasisi hiyo imesema kuwa hayo yote yanaruhusiwa kisheria, ikiongeza kuwa msingi wake unatokana na maana ya jumla ya kauli ya Mwenyezi Mungu katika Surah Yunus, aya ya 58.
"Sema: Kwa fadhila ya Mwenyezi Mungu na rehema yake! Basi nawafurahi kwa hayo. Haya ni bora kuliko hayo wanayo yakusanya."
“Aidha, kuadhimisha kuzaliwa kwa Mtume (SAW) ni kielelezo cha heshima, sherehe, na furaha kwa kipenzi chetu, Mtume Muhammad (SAW). Kusherehekea na kufurahia kumbukumbu ya siku aliyozaliwa bila shaka kunaruhusiwa, kwani kudhihirisha upendo kwake ni nguzo ya imani. Mwenyezi Mungu Mtukufu anasema: ‘Sema (Ewe Mtume): Ikiwa nyinyi mnampenda Mwenyezi Mungu basi nifuateni mimi, Mwenyezi Mungu atakupendeni na atakufutieni madhambi yenu. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kufuta madhambi na Mwenye kurehemu. (Aal-Imran: 31).’”
Taasisi hiyo imefafanua kuwa nyanja za kidini za kuadhimisha kuzaliwa kwa Mtume (SAW), ikiwemo kusoma Qur’an Tukufu, kusoma wasifu wa Mtume (Seerah), na kufanya makongamano ya dua na sifa, zote zinaruhusiwa na kupendekezwa kwa mujibu wa sheria za Kiislamu.
Dar al-Ifta imesema kuwa mojawapo ya njia bora zaidi za kusherehekea kuzaliwa kwa Mtume Muhammad (SAW) ni kumtumia swala na salamu.
“Hili hufungua milango iliyofungika, huinua daraja la mtu, na huleta utulivu wa moyo wakati wa raha na shida. Kwa hakika, (kumswalia Mtume) hutuliza kila huzuni na majonzi, hufungua vifungo, hutimiza matakwa, na kutatua shida.”
3498741