IQNA

17:17 - August 24, 2026
Habari ID: 3482671

“Ummah wa Mtume” ni Kaulimbiu Kuu ya Wiki ya Umoja wa Kiislamu

IQNA – Katibu wa Makao Makuu ya Wiki ya Umoja wa Kiislamu nchini Iran ametangaza kuwa kaulimbiu kuu ya hafla ya mwaka huu ni “Ummah wa Mtume Mtukufu (SAW).”

Hujjatul-Islam Hassan Akhtari

Katika mkutano na waandishi wa habari uliofanyika mjini Tehran siku ya Jumatatu, Hujjatul-Islam Hassan Akhtari alifafanua programu mbalimbali zilizopangwa kwa ajili ya wiki hii adhimu.

Akirejelea umuhimu wa umoja wa Ummah wa Kiislamu, alisema kuwa Wiki ya Umoja wa Kiislamu ni miongoni mwa mafanikio makubwa ya Mapinduzi ya Kiislamu, ikizingatiwa kuwa moja ya nguzo na kanuni muhimu za mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ni umoja wa Waislamu.

Huku akitoa salamu za kheri na fanaka kwa  kuingia kwa mwezi wa Rabi’ al-Awwal na matukio ya mwezi huu, ikiwemo Milad un Nabii, yaani kumbukumbu ya kuzaliwa kwa Mtume Mtukufu Muhammad (SAW), kuzaliwa kwa Imam Ja’far al-Sadiq (AS), Hijra ya Mtume Muhammad (SAW) kwenda Madina, na kuanza kwa Uimamu wa Imam wa Zama (AS), alisema kuwa Wiki ya Umoja wa Kiislamu ni fursa ya kuimarisha mshikamano na udugu miongoni mwa Waislamu ulimwenguni kote.

Akibainisha kuwa umoja wa Ummah wa Kiislamu ni moja ya mafundisho yanayosisitizwa ndani ya Qur’ani Tukufu na maisha ya Mtume Muhammad (SAW) pamoja na Ahlul-Bayt (AS), alisema kuwa baada ya kuingia Madina, Mtume (SAW) aliweka msingi wa udugu na umoja kati ya makundi mbalimbali na kuanzisha jamii ya Kiislamu kwa msingi wa mshikamano wa kweli.

Katibu huyo wa Makao Makuu ya Wiki ya Umoja wa Kiislamu ameongeza kuwa Imam Khomeini (RA) pia alichukulia suala la umoja wa Ummah wa Kiislamu kama moja ya kanuni za msingi za mfumo tangu ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu. Kwa kuitangaza Wiki ya Umoja, aliweka msingi thabiti wa mshikamano mkubwa zaidi miongoni mwa Waislamu.

Akirejelea hali ya kikanda na matukio ya sasa, Hujjatul-Islam Akhtari amesema kuwa mwaka huu, Wiki ya Umoja inafanyika wakati ambapo Ummah wa Kiislamu unakabiliwa na machungu na misukosuko mikubwa.

Amesisitiza kuwa: “Uhalifu wa utawala wa Kizayuni dhidi ya watu wa Palestina, Lebanon, na mataifa mengine ya kanda hii, pamoja na njama na fitna za maadui wa Uislamu, umeongeza maradufu haja ya kuzingatia zaidi umoja na mshikamano wa Kiislamu."

Ameongeza kuwa, “Maadui wa Uislamu wanajaribu kuleta faraka miongoni mwa Waislamu na kuchochea baadhi ya nchi za Kiislamu dhidi ya nyingine, wakitengeneza mazingira ya mgawanyiko na migogoro. Harakati za Kitakfiri pia zinafanya kazi katika mwelekeo huo huo wa kimaslahi ya maadui.”

“Kwa sababu hiyo, hali ya sasa imeipa Wiki ya Umoja ya mwaka huu sura ya kipekee na kutufanya sote tuwe na azimio zaidi la kuimarisha umoja.”

Amesisitiza jukumu la taasisi na mashirika mbalimbali katika kuendesha programu za Wiki ya Umoja, amesema: “Tunatarajia taasisi zote, wizara, mashirika, wasomi, na watu wenye ushawishi, watekeleze jukumu lao kwa juhudi zaidi katika kuimarisha umoja wa Kiislamu, tukizingatia hali ya nchi na kanda hii.”

Akibainisha programu zilizopangwa, amesema kuwa hafla kuu itakuwa ni Kongamano la 40 la Kimataifa la Umoja wa Kiislamu, litakalokuwa na mada ya: “Umoja wa Kiislamu katika Fikra za Imam Shahidi Sayyid Ali Khamenei, Bwana wa Mashahidi wa Mapinduzi ya Kiislamu.”

Siku ya 17 ya Rabi’ al-Awwal, ambayo mwaka huu inaangukia tarehe 30 Agosti, inaaminika na Waislamu wa Shia kuwa ndiyo kumbukumbu ya kuzaliwa kwa Mtume Muhammad (SAW), wakati Waislamu wa Sunni wanaamini kuwa siku ya 12 ya mwezi huo (Agosti 25 mwaka huu) kuwa ndiyo siku ya kuzaliwa kwa Mtume wa mwisho.

Muda kati ya tarehe hizo mbili ulitangazwa kuwa Wiki ya Umoja wa Kiislamu na mwanzilishi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Imam Khomeini, katika miaka ya 1980.

3498767

Habari zinazohusiana
captcha