IQNA – Kwa mnasaba wa Maulid au maadhimisho ya kuzaliwa kwa Mtume Muhammad (SAW), Kituo cha Mikutano cha Jinnah (Jinnah Conference Center) kilichopo Islamabad, Pakistan, kimeandaa kongamano la kimataifa wiki hii.
Kongamano hilo liliandaliwa na Wizara ya Masuala ya Kidini na Umoja wa Dini mbalimbali ya Pakistan, likibeba mada kuu ya “Ulinzi, Maendeleo, na Ujenzi wa Tabia ya Vijana katika Mwanga wa Sira (Wasifu) ya Mtume Muhammad (SAW)."
Lengo kuu la mkutano huo lilikuwa kuchunguza nyanja mbalimbali za maisha ya Mtume Muhammad (SAW) hususan umuhimu wa elimu ya kiakili, kimaadili, na kijamii kwa ajili ya kizazi kipya, ujenzi wa tabia, na kuimarisha uhusiano wa vijana na misingi ya Kiislamu.
Waziri Mkuu wa Pakistan, Muhammad Shehbaz Sharif, alikuwa mgeni maalum, huku Waziri wa Masuala ya Kidini na Umoja wa Dini mbalimbali, Sardar Muhammad Yousaf, akisimamia mchakato wa kongamano hilo. Mkutano ulishuhudia ushiriki mpana wa wasomi wakuu na masheikh kutoka madhehebu mbalimbali ya Kiislamu kote nchini Pakistan, pamoja na wawakilishi wa kisayansi na kijamii.
Wazungumzaji walisisitiza kuwa maisha ya Mtume Muhammad (SAW) ni chanzo kamilifu cha kuelimisha na kurekebisha maadili ya kizazi kipya na kujenga jamii yenye usalama, utulivu, na uadilifu. Walihimiza haja ya kupata msukumo kutoka kwa mwenendo wa Mtume katika kukabiliana na changamoto za kiakili na kimaadili zinazokabili vijana wa sasa.
Maulana Muhammad Abdul Khabir Azad, Imamu wa Msikiti wa Mfalme wa Lahore, alihutubia kongamano hilo kuhusu umuhimu wa kuelimisha vijana kwa kufuata mwongozo wa Mtume, kuimarisha umoja wa kitaifa, na kueneza maadili ya amani na uvumilivu.
Washiriki walisisitiza kuwa changamoto nyingi za sasa zinazokikabili kizazi kipya zinahitaji kurudi kwenye mafundisho ya maisha ya Mtume (SAW) na kuyafanya kuwa mwongozo wa kivitendo wa maisha. Walithibitisha kuwa maisha ya Mtume (SAW) ni mfano kamili wa uadilifu, rehema, upendo, na udugu.
Kongamano lilihitimisha kwa kusisitiza kuwa Sira ya Mtume (SAW) si simulizi ya kihistoria tu, bali ni mbinu jumuishi na ya kivitendo ya kujenga mtu binafsi, familia, na jamii, na kukuza maadili katika maisha ya kisasa.
3498810