IQNA

17:07 - August 29, 2026
Habari ID: 3482690

Sheikh Naim Qassem: Umoja wa Kiislamu ni ngao ya kulinda Umma na Mhimili wa Ukombozi wa Palestina

IQNA: Sheikh Naim Qassem alitoa kauli hiyo katika hotuba aliyoitoa Ijumaa usiku, katika kuadhimisha kumbukumbu ya Maulid ya Mtume Mtukufu (SAW) na Imam Ja’far al-Sadiq (AS), sambamba na Wiki ya Umoja wa Kiislamu (Wiki ya Wahda).

Naim Qassim

Alikuwa akilihutubia hadhira katika hafla iliyoandaliwa kwa mnasaba huo viungani mwa mji mkuu wa Beirut kusini mwa Lebanon (Dahiya).

Sheikh Qassem alieleza kuwa umoja wa Kiislamu unaokusudiwa na kutamaniwa ni ule unaoleta izza, mamlaka, na kinga thabiti kwa Waislamu, huku ukichochea maendeleo na ushirikiano baina yao, hususan kati ya serikali na mataifa mbalimbali.

“Umoja wa Kiislamu unahitajika ili kuukomboa Umma kutoka kwenye utegemezi na kujiangamiza wenyewe, sambamba na kukabiliana na fitina pamoja na vikwazo vya kidini, kimadhehebu na kisiasa; na maana yake hasa ni kuelekeza macho na nguvu zote kwa adui wa kweli wa Umma na kujiondoa kwenye migogoro na hitilafu za ndani,” alisema Sheikh Qassem.

Kiongozi huyo Mkuu wa Hizbullah alibainisha kuwa umoja wa Kiislamu una matokeo makuu mawili: “Matokeo ya kwanza ni kwamba tunaungana ili kuzuia na kuzima fitina, na kwamba umoja huu unapanuka hadi kuwa umoja wa kitaifa na wa kibinadamu. Matokeo ya pili ni kuwa tunaungana na kushikamana kikamilifu kuzunguka kadhia ya msingi, nayo ni kadhia ya Palestina, ambayo inabeba na kuwakilisha mustakabali wa eneo zima.”

Aliongeza kuwa suala la Palestina si suala la kidini tu, bali ni kadhia ya Kiislamu, ya kitaifa, ya Kiarabu, na ya kibinadamu kwa ujumla, na inapasa iwe ndio mhimili mkuu wa umoja wa Umma wa Kiislamu.

Sheikh Qassem alisisitiza: “Tunatoa wito kwa nchi za Kiarabu na za Kiislamu pamoja na mataifa yao kuungana na kutokuwa watazamaji tu mbele ya kuingiliwa kwa eneo letu na maadui, wala mbele ya dhiki, mateso na mashaka wanayopitia ndugu zao.”

Alisema kuwa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran pamoja na vikosi vya Muqawama (Mapambano ya Kiislamu) vinakabiliana kishujaa na njama za muungano wa Marekani na Uzayuni, na akasisitiza kuwa wakati umefika kwa eneo hili kupata usalama wa kudumu na kukomesha ubeberu na kiburi cha kiistikbari kupitia maelewano na maridhiano baina ya nchi za ukanda huu.

Kwingineko katika hotuba yake amesema: Wanamapambano wa harakati ya Hizbullah ya Lebanon wamefanikiwa kuzima njama iliyopewa jina la "Israel Kubwa" na kuzuia upanuzi wa Israel hadi Lebanon. Haya yamesemwa na Katibu Mkuu wa harakati hiyo ya Lebanon.

 Sheikh Naim Qassem amesema kuwa Washington na utawala wa Tel Aviv zinaandaa mradi kabambe kwa lengo la kuimarisha uvamizi, kukalia kwa mabavu na kuligawa eneo la Asia Magharibi."Washington inaanda msingi wa kutekelezwa mpango wa 'Israeli Kubwa' kwa kutumia uwezo wake wa kijeshi.  Hata hivyo, Iran na vikosi vya wanamuqama kote katika eneo hili vinapinga mpango huo," ameeleza Katibu Mkuu wa Hizbullah ya Lebanon.Sheikh Qassim ameesema kuwa kujitoa mhanga kulikofanywa Palestina, Lebanon, Iran, Yemen na Iraq kumesimamisha mradi huo, na kusisitiza kuwa Mhimili wa Muqawama unaendelea kustawi licha ya hasara zilizopatikana katika mapambano dhidi ya utawala ghasibu wa Israel.Ameongeza kuwa matukio yanayoendelea nchini Syria ni uthibitisho mwingine wa jitihada za Marekani na Israel za kuendeleza mradi wa ‘Israel Kubwa’.Neno "Israel Kubwa" limekuwa likitumika tangu Vita vya Waarabu na Israel mwaka 1967 kuelezea maeneo yanayokaliwa kwa mabavu na Israel, ikiwa ni pamoja na Jerusalem Mashariki (al-Quds), Ukingo wa Magharibi, Ukanda wa Gaza, Peninsula ya Sinai ya Misri na Milima ya Golan ya Syria yenye umuhimu wa kimkakati.

/3498818

Habari zinazohusiana
captcha