IQNA

18:00 - August 29, 2026
Habari ID: 3482691

Serikali ya Uingereza Yasukumwa Kuchukua Hatua Kulinda Misikiti Huku Chuki Dhidi ya Uislamu na Undumakuwili wa Kisera Vikiongezeka

IQNA-Viongozi wa Waislamu na Jukwaa la Jumuiya za Kiislamu (FMO) katika eneo la Greater Manchester wameitaka serikali ya Uingereza kuchukua hatua za dharura na kutoa fungu maalum la fedha za ulinzi wa Waislamu na misikiti kufuatia kutiwa hatiani kwa Gabriel Levy kijana Yahudi mwenye umri wa miaka 21.

Gabriel Levy

Levy alihukumiwa kifungo cha miezi 28 jela katika Mahakama ya Leeds Crown baada ya kukiri kutoa vitisho vya mauaji vya chuki dhidi ya Uislamu (Islamophobia) kwa waumini wa Misikiti ya Al-Sunnah na Iqra mnamo Oktoba 2025. Uchunguzi wa simu yake ulifichua lugha chafu za kibaguzi na chuki dhidi ya Uislamu. Idara ya Mashtaka (CPS) ilieleza kuwa vitisho hivyo vilifuatia shambulio kwenye sinagogi moja la eneo hilo, licha ya kuwa jamii ya Kiislamu iliyolengwa haikuwa na uhusiano wowote na tukio hilo.

Jukwaa la FMO lilisisitiza kuwa vitisho dhidi ya misikiti vinatia hofu mamia na maelfu ya waumini wanaotaka kuswali kwa amani, huku likibainisha kuwa wimbi la chuki dhidi ya Uislamu nchini Uingereza limefikia kiwango cha juu zaidi katika historia. Takwimu kutoka Taasisi ya Waislamu wa Uingereza (British Muslim Trust) zinaonyesha kuwa kwa wastani msikiti mmoja hushambuliwa kila baada ya siku tano nchini humo, kukiwa na zaidi ya matukio 70 ya uvamizi, vitisho na uchomaji moto katika kipindi cha miezi 12, ikiwemo mashambulizi ya mara kwa mara kwenye Kituo cha Kiislamu cha Nasfat mjini Manchester na kutupwa bomu la moto kwenye nyumba ya imamu mmoja huko Bolton.

Waislamu walieleza kutoridhishwa kwao na ucheleweshaji wa urasimu wa mpango wa Wizara ya Mambo ya Ndani wenye thamani ya pauni milioni 40 unaokusudiwa kuimarisha usalama wa misikiti, hali inayoiacha nyumba nyingi za ibada katika hatari kubwa huku zikingojea msaada kwa miezi kadhaa.

Aidha, wanaharakati na wachambuzi wameukosoa undumakuwili wa wazi wa serikali na vyombo vya habari vya Magharibi. Wakati shambulio la uchomaji wa magari ya wagonjwa ya jamii ya Kiyahudi ya Hatzola mnamo Machi 2026 lilipokelewa kwa matamko ya haraka bungeni, fidia ya serikali, na bajeti ya ulinzi wa pauni milioni 59, mashambulizi dhidi ya taasisi za Kiislamu yamepuuzwa. Vyombo vya habari pia vimeonyesha upendeleo kwa kufunika kesi ya Levy kimyakimya bila uchambuzi wa kina, kinyume kabisa na jinsi vinavyoendesha kampeni chafu za upotoshaji pindi mtuhumiwa anapokuwa Mwislamu.

/3498820

captcha