IQNA – Hafla kubwa ya kipekee ilifanyika katika Kaburi Tukufu, yaani Haram ya Imam Ali (AS) mjini Najaf, Iraq, ambapo bendera maalum ya kuadhimisha kumbukumbu ya kuzaliwa kwa Mtume Muhammad (SAW) na Imam Ja’far al-Sadiq (AS) ilipeperushwa kwa taadhima.
Kwa mujibu wa Mtandao wa Haram ya Imam Ali (AS), hafla hiyo ilihudhuriwa na Katibu Mkuu wa Astan (Idara ya Mfawidhi) wa eneo hilo tukufu, Sayid Isa Khorasan, na naibu wake, wajumbe wa Bodi ya Wakurugenzi ya Astan, Gavana wa mkoa wa Najaf, pamoja na makamanda mbalimbali wa usalama, maafisa wa serikali, na watu mashuhuri wa kijamii.
Haider al-Issawi, mjumbe wa Bodi ya Wakurugenzi ya Astan, katika hotuba yake kwa niaba ya sekretarieti ya Astan, alisema kuwa hafla hii inadhimisha kuzaliwa kwa viongozi wawili mbarikiwa ambao walimulika njia ya historia na ubinadamu kwa ujumla. Alibainisha kuwa hawa viongozi wakuu wawili walikuwa wajumbe wa dhana za rehema, uongofu, na elimu ya kweli.
Katika kipindi cha sherehe hizo, kulikuwa na programu za sherehe na nyimbo za kusifu (nasheed) ambazo zilikuwa ni ishara ya furaha na bashasha ya waumini kwa ajili ya tukio hili lenye baraka tele.
Aidha, hafla hiyo ilizindua kuanza kwa Wiki ya Tano ya Kimataifa ya “Sadiqeen”, ambayo inajumuisha mfululizo wa programu mbalimbali za aya za Qur’ani, utamaduni, sayansi, mijadala, ushairi, pamoja na matukio ya kijamii na kuadhimisha watu mashuhuri. Programu hizo zitaendeshwa katika maeneo ya karibu na Makabrini Matukufu ya Imam Ali (AS) na sehemu nyingine mbalimbali mjini Najaf. Programu za tukio hili pia zimepanuka hadi maeneo mengine ndani ya Iraq na hata nje ya mipaka ya nchi.
Kwa mujibu wa aghalabu ya riwaya za Madhehebu ya Shia Ithnaashariya, Mtume Muhammad (SAW) alizaliwa tarehe 17 ya mwezi wa Rabi al-Awwal. Tarehe hiyo pia inadhimisha kuzaliwa kwa Imam Sadiq (AS). Tarehe 17 ya Rabi al-Awwal mwaka huu inaangukia siku ya Jumapili, Agosti 30. Waislamu wa madhehebu ya Sunni huamini kuwa Mtume Muhammad (SAW) alizaliwa tarehe 12 Rabi al-Awwal. Kipindi cha baina ya tarehe hizo mbili kilitangazwa na Imam Khomeini (MA), muasisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, kuwa Wiki ya Umoja wa Kiislamu na hivyo nukta ya hitilafu ikageuzwa kuwa nukta ya umoja.
3498819