IQNA – Naibu Katibu Mkuu wa harakati ya Jihad al-Islami ya Palestina amesema kuwa mfumo wa kimataifa unaoegemea kwenye ubeberu na utawala wa Marekani uko katika hali ya mmomonyoko wa wazi na unashuhudia mgongano endelevu wa kimaslahi kati ya madola makubwa.
“Uongo wa Marekani kuhusu madai ya kuzilinda nchi nyingine na falsafa ya kuanzisha kambi zake za kijeshi umefichuliwa wazi wakati wa vita vya hivi karibuni. Je, kuna faida gani ya kambi hizi ambazo mabilioni ya dola yametumika kuziunda?” Muhammad Al-Hindi alinukuliwa akisema na shirika la habari la Palestine Today.
Aliongeza kuwa matokeo ya mzozo wa sasa yataunda mustakabali wa kisiasa wa eneo hili kwa miongo kadhaa ijayo, sawa na yale yaliyotokea mnamo mwaka 1948.
Alisisitiza kuwa taifa la Palestina, ambalo linakabiliwa na uvamizi na uchokozi endelevu, halihitaji ruhusa ya mtu yeyote ili kudai haki yake.
“Nchi za Kiarabu na Kiislamu zimeiacha Palestina peke yake, na wakazi wa Ukanda wa Gaza wamevumilia kwa muda mrefu, na sasa hawawezi tena kuvumilia mauaji, njaa, na udhalilishaji zaidi.”
Al-Hindi alisema mashauriano kati ya makundi na mirengo ya Palestina yanaendelea kwa lengo la kuunga mkono orodha moja ya kitaifa na kuunganisha safu ili kukabiliana na changamoto zilizopo.
Aliongeza: “Uchaguzi wa sasa haujibu matakwa ya wananchi wa Palestina, bali unanyakua haki ya watu ya kujiamulia mambo yao wenyewe.”
Alibainisha kuwa Jihad al-Islami imetoa wito wa kuahirishwa kwa uchaguzi huo hadi makubaliano ya kina yatakapofikiwa ili kurekebisha na kuunda upya Harakati ya Ukombozi wa Palestina (PLO).
Alimalizia kwa kusema kuwa harakati ya Jihad al-Islami haitakuwa na wagombea wowote katika uchaguzi huo, lakini itaiunga mkono orodha yoyote ambayo itafikiwa kwa makubaliano ya kitaifa.
4372579