IQNA-Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Sayyid Mojtaba Khamenei amesema, watawala wahalifu na watenda jinai wa Marekani na wa utawala wa Kizayuni si maadui wa taifa la Iran peke yake, bali ni maadui pia wa Umma mzima wa Kiislamu huku akisisitiza kuwa, dawa ya matatizo ya Umma wa Kiislamu ni umoja na urafiki.
Ayatullah Khamenei amebainisha hayo katika ujumbe maalumu aliotoa leo Jumapili kwa mnsaba wa Maulid ya Mtume Muhammad (SAW) na maadhimisho ya Wiki ya Umoja wa Kiislamu.
Katika ujumbe wake huo, Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amewaasa watawala wa nchi za Kiislamu, hususan wa nchi za Asia Magharibi na eneo la Ghuba ya Uajemi wamjue adui yao halisi, na kutambua pia njama zake na kukabiliana nazo.
"Dawa ya matatizo ya Umma wa Kiislamu inapatikana kwenye kalima ya umoja, urafiki, na ushirikiano katika kufanya kheri na mema," ameeleza Ayatullah Khamenei.
Amesema: "Watawala wahalifu wa Marekani na wa utawala bandia wa Kizayuni ni maadui walioukamia umoja na urafiki huu. Wao si maadui wa Jamhuri ya Kiislamu, taifa la Iran, na kambi kubwa ya Muqawama wa Kiislamu tu; bali ni maadui kwa Umma mzima wa Kiislamu, ikiwa ni pamoja na mataifa ya Asia Magharibi na Afrika Kaskazini; na katika suala hili, hata watawala wa nchi hizo , ambao wengi wao wanahesabiwa kuwa washirika wao, nao pia hawajaachwa. Mngali mnakumbuka nyinyi na sisi uvunjiaji heshima wa hadharani na utumiaji misamiati michafu uliofanywa na viongozi wa madola ya kibeberu kwa baadhi ya viongozi wa nchi za Kiislamu".
Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amebainisha katika ujumbe wake kwamba suala la umoja miongoni mwa Waislamu linacho kigezo na mfano mzuri wa kuiga kwa wananchi wa Iran, ambapo njama za maadui hazijaweza kuwa na athari kubwa za kuudhoofisha umoja wao. Pamoja na hayo ametanabahisha kwa kusema:
"Lakini bila shaka yoyote, wanaotutakia mabaya wanainyemelea neema hii kubwa. Kinachowapa wao matumaini ni kuzikuza tofauti. Japokuwa tofauti za kiitikadi na kimadhehebu ni sehemu muhimu ya kile ambacho maadui wa Uislamu wamekusudia kukitumia na wameelekeza matumaini makubwa kwenye hilo, lakini hawatakomea hapo. Watafanya kila njia kutumia visingizio vya tofauti za kikabila, kitamaduni, kijamii, kiuchumi, kisiasa, na kijiografia ili kuzusha mifarakano baina ya Waislamu ndani ya Iran na katika kila nchi nyingine ya Kiislamu, ili kuuona Umma wa Kiislamu unavyopasuka vipande vipande na kudhoofika nguvu zake na kusubiri itapopatikana fursa mwafaka waweze kuutawala."
Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu ameukumbusha Umma wa Kiislamu kwamba hivi sasa ni wakati muafaka kwa Waislamu kutafakari kwa kina na kuchunguza kwa makini zaidi matukio yanayojiri na akahoji:
"Kama Waislamu wangesimama pamoja wakiwa wamekunja ngumi zao barabara, je, taifa la Palestina lingebaki bila ya hifadhi na ulinzi, likiandamwa na dhulma na jinai za maghasibu? Na lau kama wananchi na serikali za nchi zinazopakana na Ghuba ya Uajemi wangejenga umoja wao chini ya bendera ya Uislamu, je, genge la watu wasio na utambulisho na mafisadi wangethubutu kuja kutokea umbali wa maelfu ya kilomita kwa tamaa ya kupora ardhi na mali zao?"
Aidha amesisitiza kuwa "umoja na kuepuka mifarakano" ni somo la kwanza la njia ya fikra ya Uislamu kwa ajili ya kuamiliana na adui na rafiki; na kwamba "somo la pili ni kila Muislamu kumhami Muislamu mwenzake dhidi ya ukafiri; na somo la tatu ni Waislamu kushirikiana katika nyanja tofauti za maisha ya kimaada na kiroho, kwa upande wa mali na utajiri, usalama, elimu na maendeleo, ambapo kilele cha njia hiyo kitakuwa ni kuufikia Ustaarabu mpya wa Kiislamu.
3498834