IQNA – Msomi na mwanafalsafa wa Kiislamu kutoka Guinea amesisitiza kuwa umoja wa Kiislamu si kaulimbiu ya kisiasa, bali ni ulazima wa dharura kwa ajili ya usalama na ustawi wa Ummah katika ulimwengu wa sasa uliokumbwa na misukosuko.
“Ni jukumu letu kama watafiti na waelimishaji kutekeleza majukumu yetu ya kisayansi na kivitendo katika kuufikisha ujumbe wa Uislamu wa kweli kwa kila mtu kwa njia iliyo sahihi na yenye ufanisi,” alisema Sheikh Moussa Bawaro, Makamu wa Rais wa Umoja wa Kitaifa wa Walinganizi (Da’wah) nchini Guinea, katika mahojiano na Katika mahojiano na Shirika la Habari za Qur'ani la Kimataifa (IQNA) pembezoni mwa Mkutano wa 40 wa Kimataifa wa Umoja wa Kiislamu, uliofanyika mjini Tehran wiki iliyopita.
Hapa chini ni muhtasari wa mahojiano hayo:
IQNA – Nini suluhisho la kufikia amani na usalama wa kudumu na kuutayarisha Ummah wa Kiislamu kukabiliana na changamoto za kikanda na kimataifa?
Sheikh Bawaro: Mtazamo wangu ni kuwa jibu linapatikana katika kurejea kwa Qur’ani Tukufu na mwongozo wa wazi wa Mtume Muhammad (SAW). Kwanza, katika Qur’ani Tukufu, Mwenyezi Mungu anawahutubia Waislamu wote: “Na shikamaneni kwa kamba ya Mwenyezi Mungu nyote pamoja, wala msifarakane” (Surah Al-Imran, 103). Hii inamaanisha kuwa Waislamu wote ni lazima wawe wamoja na washikamane kwa pamoja kwenye kifungo kimoja hicho, yaani, kamba ya Mwenyezi Mungu.
Hii inatuongoza kwenye yale ambayo Mtume Muhammad (SAW) alituita tufanye; ambapo alisema: “Hapana mmoja wenu atakayekuwa na imani ya kweli mpaka ampendelee ndugu yake kile anachojipendelea yeye mwenyewe.” Unanipenda na unamtakia ndugu yako Muislamu kile unachojitakia wewe mwenyewe. Na Mtume (SAW) pia amesema katika hadithi nyingine: “Muumini kwa muumini mwingine ni kama jengo ambalo sehemu zake huungana na kusaidiana.”
Katika hadithi nyingine, Mtume (SAW) alielezea waumini katika nuru ya upendo wao na mshikamano wa pamoja na kuifananisha jamii nzima ya Kiislamu na mwili mmoja: “Wakati wowote kiungo kimoja cha mwili huu kinapoumia na kupata maumivu, viungo vingine humwitikia kwa kukosa usingizi na homa.” Kwa hiyo, tunauitolea wito Ummah wa Kiislamu duniani kote kudumisha umoja na uadilifu. Ikiwa, Mungu apishe mbali, madhara yatamfika Muislamu nchini Iran, Palestina, au Guinea-Bissau, jamii nzima ya Kiislamu katika kila pembe ya dunia inapaswa kuhisi kama janga hilo limewapata wao wenyewe binafsi.
IQNA – Kwa maoni yako, je, dhana ya umoja wa Kiislamu na kuimarisha maelewano kati ya madhehebu ya Kiislamu inamaanisha kuacha itikadi au imani zetu, au inamaanisha kitu kingine?
Sheikh Bawaro: Umoja wa Kiislamu haumaanishi kuacha itikadi, kwa sababu hatutofautiani sana katika misingi yetu ya kiimani. Tofauti zilizopo kati ya mbinu mbalimbali za Kiislamu ni katika matawi na maelezo tu, wakati tunakubaliana katika nguzo na misingi ya dini kama vile swala, saumu, Hija, Qur’ani na utume. Tofauti za maoni hutokea tu katika tafsiri ya maandiko na dhana zilizo nje ya misingi hii mikuu. Kwa hiyo, mimi siungi mkono kuacha imani za msingi au asili ya dini na kusababisha migawanyiko kwa kisingizio cha mambo ya kidini.
IQNA – Kwa maoni yako, nini wajibu wa wanazuoni, wahariri wa vyombo vya habari, na wasomi katika ulimwengu wa Kiislamu ili kuzuia migawanyiko na matusi dhidi ya matukufu ya wafuasi wa madhehebu mbalimbali ya Kiislamu?
Sheikh Bawaro: Kufikisha ujumbe wa Uislamu ni wajibu wa imani, sharti la kisayansi na ulazima wa Kiislamu kwa wakati mmoja. Jukumu la kuufikisha ujumbe wa kweli wa Uislamu kwa ulimwengu mzima – kwa Waislamu na wasio Waislamu – limewekwa juu yetu. Ni jukumu letu kama watafiti, waelimishaji, na walimu, kuufikisha ujumbe huu adhimu na wa kweli kwa kila mtu kwa njia iliyo sahihi na yenye ufanisi.
3498845