IQNA-Jeshi la Iran la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran limetangaza kuwa Kikosi chake cha Anga kimeshambulia maeneo na kambi za kijeshi za Marekani huko Jordan, na kutoa jibu la haraka kwa shambulio la kigaidi la Marekani katika Kisiwa cha Larak nchini Iran jana usiku.
IRGC imeeleza katika taarifa yake leo asubuhi kwamba operesheni ya pamoja iliyohusisha makombora na ndege zisizo na rubani iliyopewa jina la "Adhabu kwa Mchokozi," imezilenga kambi za kijeshi za King Hussein na Al-Azraq ambazo zimewapa hifadhi wanajeshi wa Marekani.
Operesheni hiyo imeilenga "miundombinu ya kiufundi na ya ukarabati, pamoja na maeneo ya kuegeshea ndege za kivita za adui," na kusababisha uharibifu mkubwa kwa rasilimali za kijeshi za adui mchokozi.
IRGC imebainisha kuwa shambulio hilo ni jibu la lazima na halali dhidi ya shambulio la jana usiku katika Kisiwa cha Larak katika Lango la Bahari la Hormuz, ambalo limeuwa shahidi na kuwajeruhi wanajeshi na raia kadhaa wa Iran.
"Vitendo vya uchokozi na jinai havitatatua kukata tamaa kwa adui katika jaribio lake la kudhoofisha udhibiti wa Jamhuri ya Kiislamu kwa Lango la Bahari la Hormuz, na kila shambulio litajibiwa kwa hatua kali zaidi na zenye madhara makubwa," imeeleza taarifa ya Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran.
Operesheni ya leo asubuhi ya IRGC dhidi ya kambi za kijeshi zinaowahifadhi wanajeshi wa Marekani huko Jordan inasisitiza msimamo thabiti wa Iran kwamba shambulio lolote dhidi ya ardhi ya Iran hasa katika maeneo ya kimkakati ya Ghuba ya Uajemi na Lango la Hormuzlitajibiwa kwa namna hiyo hiyo na kwa nguvu kubwa zaidi.
Wakati huo huo, Jeshi la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran latangaza operesheni ya droni dhidi ya kambi ya kijeshi ya Marekani nchini Imarati (UAE) ikiwa ni jibu kwa shambulio la Marekani katika Kisiwa cha Larak
Jeshi la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran limetangaza operesheni ya droni inayowalenga wanajeshi wa Marekani walioko katika kituo kimoja cha kijeshi nchini Imarati (UAE), ikiwa ni malipizi ya shambulio la kikatili la Marekani dhidi ya Kisiwa cha Larak katika Mlango-Bahari wa Hormuz.
Katika taarifa iliyotolewa Jumatatu asubuhi, jeshi hilo limesema kuwa shambulio hilo lilihusisha makumi ya droni za kujitolea mhanga , na kulenga maeneo yanayohifadhi helikopta za kijeshi na wanajeshi wa Marekani katika Kituo cha Anga cha al-Minhad, kilichopo takriban kilomita 24 kusini mwa Dubai.
Taarifa hiyo iliongeza kuwa operesheni hiyo ilikuwa ni jibu kwa shambulio la Marekani la usiku wa Jumapili dhidi ya Kisiwa cha Larak, ambalo lilisababisha vifo na majeraha kwa wanajeshi kadhaa wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) pamoja na raia wa kawaida.
Jeshi la Iran limesema Kituo cha Anga cha al-Minhad ni kituo muhimu cha usafirishaji wa vifaa vya kijeshi na anga kwa vikosi vya kigeni, na kuahidi kuendeleza operesheni zaidi za kulipiza kisasi dhidi ya wanajeshi wa Marekani.
“Vikosi vya Jeshi la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran vinasalia imara katika kuhakikisha usalama wa kudumu na kulinda ardhi ya Iran hadi pale tishio la adui litakapoondolewa katika eneo hili,” taarifa hiyo ilisisitiza.
Iliongeza kuwa jeshi hilo litalipiza kisasi cha damu ya mashahidi wote wa vita vya kulazimishwa kwa kukabiliana na “vikosi vya kigaidi vya Marekani.”
3498843