IQNA – Awamu ya tatu ya Siku ya Kimataifa ya Usomaji wa Qur’ani Tukufu imezinduliwa rasmi mjini Cairo, mji mkuu wa Misri, Jumapili asubuhi.
Hafla hiyo iliyoandaliwa na Kurugenzi Kuu ya Masuala ya Qur’ani katika Taasisi za Al-Azhar, ilizinduliwa chini ya udhamini na usimamizi wa Sheikh Ahmed Al-Tayeb, Imamu Mkuu wa Al-Azhar.
Mpango huo umeleta pamoja mamia ya maelfu ya wasomaji (Qurraa) wa Qur’ani kutoka kote nchini Misri na mataifa mengi duniani.
Sheikh Ayman Abdel-Ghani, Naibu Mkuu wa Al-Azhar, alisisitiza kuwa tukio hili linawakilisha fursa muhimu ya kuhuisha uhusiano na Qur’ani Tukufu na kuziunganisha familia na vizazi mbalimbali chini ya mafundisho yake.
Alieleza kuwa wigo mpana wa mpango huu katika ngazi ya ndani na kimataifa unaonyesha nafasi ya uongozi ya Al-Azhar katika kulitumikia Kitabu cha Mwenyezi Mungu, pamoja na kujitolea kwake bila kuyumba katika kupandikiza maadili na nidhamu za Qur’ani katika nyoyo za Ummah.
Ahmed El-Sharkawy, Mkuu wa Sekta ya Taasisi za Al-Azhar, alieleza kuwa Siku ya Kimataifa ya Usomaji wa Qur’ani inakuja kama kilele cha juhudi endelevu za kuwahimiza vijana kuhifadhi na kumudu usomaji bora wa Qur’ani Tukufu.
Abu El-Yazid Salama, Mkuu wa Kurugenzi Kuu ya Masuala ya Kielimu katika Sekta ya Taasisi za Al-Azhar, alisema maandalizi ya tukio hili yalijumuisha uundaji wa mpango kamili na ulioratibiwa kwa makini ili kurahisisha ushiriki wa idadi kubwa ya wasomaji na walimu wa kuhifadhisha Qur’ani katika maeneo mbalimbali.
Awamu ya mwaka huu inaashiria hatua kubwa na upanuzi wa kipekee katika wigo wa ushiriki. Msikiti wa Al-Azhar umefungua milango yake kupokea wasomaji kutoka taasisi za Al-Azhar za ndani ya Misri na nje ya nchi, pamoja na matawi ya Umoja wa Kimataifa wa Wahitimu wa Al-Azhar nchini Misri na kote duniani.
Toleo hili la tatu pia limetofautiana kwa ushiriki wa dhati na uratibu wa karibu na Wizara ya Wakfu ya Misri, Wizara ya Umoja wa Jamii, Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali, Taasisi ya kutoa Fatwa ya Misri (Dar al-Ifta), pamoja na mashirika ya kiraia. Ushirikiano huu unaonyesha juhudi za pamoja za taasisi za dola katika kuwahimiza watoto na vijana kuhifadhi, kumudu vyema, na kutafakari maana za Qur’ani Tukufu.
Mpango huu umeendelea kukua kwa kasi kubwa kwa mwaka wa tatu mfululizo. Ulianza na takriban washiriki 6,000 katika awamu yake ya kwanza, ukavuka washiriki 100,000 katika mwaka wake wa pili, na sasa umepanuka na kupata ushiriki mkubwa kitaifa na kimataifa.
3498846