IQNA

19:10 - September 01, 2026
Habari ID: 3482703

Binti wa miaka 17 ashtakiwa Marekani kwa kuhusika katika shambulizi la kigaidi dhidi ya Msikiti San Diego

IQNA – Mahakama ya Hakimu Mkazi katika jimbo la North Carolina, Marekani, imemfungulia mashtaka rasmi binti mmoja mwenye umri wa miaka 17; si kwa kufyatua risasi, bali kwa kushika kamera na kurekodi jinai hiyo ya kigaidi.

V

Baraza Kuu la Mahakama (Grand Jury) katika jimbo hilo lilimfungulia mashtaka binti huyo siku ya Jumatatu kwa tuhuma za kusaidia na kuwezesha kutekelezwa kwa shambulizi la umwagaji damu lililotokea Mei 18 katika msikiti mmoja mjini San Diego, ambapo Waislamu watatu waliuawa shahidi. Binti huyo anatuhumiwa kurusha mubashara (live streaming) na kusambaza video ya mashambulizi hayo ya kinyama mtandaoni.

Mwendesha Mashtaka wa Kaunti ya Forsyth, Jim O’Neill, aliwaambia wanahabari kuwa mamlaka ziliamua kumfungulia mashtaka chini ya sheria za jimbo kwa sababu sheria za North Carolina zinaruhusu mshtakiwa huyo kuhukumiwa kama mtu mzima. Iwapo atapatikana na hatia, anakabiliwa na adhabu ya kifungo cha maisha jela bila msamaha, tofauti na mashtaka ya serikali kuu (federal) ambayo yangempa kifungo cha miaka mitatu au minne pekee.

Waumini hao watatu waliouawa shahidi katika shambulizi hilo wamesifiwa kwa ushujaa wao wa kukabiliana na magaidi hao na kuzuia maafa makubwa zaidi, wakati huo kukiwa na watoto 140 ndani ya shule ya msikiti huo. Mashahidi hao, mlinzi Amin Abdullah (miaka 51), mtunza msikiti Mansour Kaziha (miaka 78), na Nadir Awad (miaka 57), ambaye alikuwa mume wa mwalimu katika Kituo cha Kiislamu cha San Diego (Islamic Center of San Diego), walitukuzwa kama mashujaa katika hafla ya kumbukumbu na maombolezo.

Washambuliaji hao wenye itikadi kali za chuki dhidi ya Uislamu (Islamophobia), Caleb Vazquez (miaka 18) na Cain Clark (miaka 17), walijiua kwa kujipiga risasi ndani ya gari lao walipokuwa wakikimbia eneo la tukio. Wachunguzi wameeleza kuwa magaidi hao pia walikuwa na mpango wa kushambulia sinagogi la Kiyahudi pamoja na shule ya upili inayotawaliwa zaidi na wanafunzi wenye asili ya Kiafrika (Wamarekani Weusi).

Mshtakiwa huyo, Sarah Lindsey Santiago, alikamatwa wiki iliyopita. Hati ya mashtaka iliyotolewa siku ya Jumatatu inamtuhumu kwa makosa matatu ya mauaji ya kukusudia na kosa moja la kula njama za kutenda uhalifu.

Shirika la habari la Reuters halikufanikiwa kumpata wakili yeyote anayemtetea Santiago.

Mwendesha Mashtaka O’Neill alieleza kuwa mtu anaweza kupatikana na hatia ya kusaidia na kuwezesha jinai iwapo anashiriki nia ovu (criminal intent) sawa na wahalifu wakuu na akashindwa kutoa msaada kuzuia uhalifu huo, hata kama hakuwepo kimwili eneo la tukio.

Kabla ya shambulizi hilo, Santiago alikubaliana na wauaji hao kurusha mubashara tukio hilo, kulisambaza hadharani mitandaoni, kisha kutoa waraka wenye itikadi na ilani yao ya chuki (manifesto) ili kuhalalisha ugaidi huo, ilieleza taarifa ya ofisi ya O’Neill.

O’Neill aliwaelezea watuhumiwa hao kama sehemu ya “kikundi cha siri chenye itikadi kali” kinachowapotosha na kuwatia kasumba vijana kufanya jinai za kutisha.

“Ni mtandao uliojaa chuki kali dhidi ya tamaduni na dini mbalimbali. Kulingana na ilani yao, Clark na Vazquez wanaonekana kuchukia kila mtu, bila kujali rangi ya ngozi, mrengo wa kisiasa, dini, au kabila. Katika mtandao huu wa chuki ya chinichini, wanasikilizana na kuwasiliana kupitia majukwaa yaliyolindwa kwa njia fiche ya kidijitali,” alisema O’Neill.

Wachunguzi wamebaini kuwa watu watatu walikuwa wakitazama shambulizi hilo moja kwa moja (livestream) wakati likiendelea, alisema O’Neill. Hapo awali walimtambua mwanamke mmoja tu aliyekuwa katika ukanda wa saa za Mashariki (Eastern time zone), na baadaye wakathibitisha kuwa ni Santiago. Mwendesha mashtaka alikataa kubainisha iwapo watu wengine wawili waliokuwa wakitazama video hiyo wametambuliwa au kama nao watafunguliwa mashtaka.

3498859

Habari zinazohusiana
captcha