IQNA – Kituo kipya cha mafunzo na kuhifadhisha Qur’ani Tukufu kwa wanawake kiitwacho Kituo cha Maryam Bint Muhammad Bin Eid Al-Muhannadi kimefunguliwa rasmi katika mji wa Al Khor, nchini Qatar.
Kituo hiki kinalenga kueneza na kuimarisha elimu ya Qur’ani Tukufu, kulea na kusimika maadili ya Kiislamu, kuimarisha utambulisho wa kitaifa na kidini kwa vizazi vijavyo, pamoja na kutoa mazingira maalum na tulivu ya kielimu kwa wanawake na wasichana wa mji huo na maeneo ya jirani.
Kituo hicho kinatoa programu mbalimbali na halqa (duru za masomo) za Qur’ani kwa makundi ya rika na viwango tofauti vya kielimu, kikiwawezesha wanafunzi kunufaika na mitaala iliyoandaliwa mahsusi kulingana na mahitaji na uwezo wao binafsi.
Programu za kituo hicho zinajumuisha hifdhi ya Qur’ani (kuhifadhi kwa moyo), marudio (Muraja’ah), kuboresha na kumudu usomaji fasaha (Tilawah na Tartil), mafunzo ya kanuni za Tajweed, sambamba na tadabburi (kuzingatia na kutafakari maana na mafunzo ya aya tukufu) pamoja na kuunganisha miongozo hiyo ya Qur’ani na matendo na maisha ya kila siku.
Kituo cha Al-Muhannadi pia kitaweka nguvu kubwa katika kubuni programu mbalimbali za kielimu na kimaadili zinazofungamana na Qur’ani, pamoja na kuajiri wanazuoni na walimu wabobezi katika fani ya kufundisha Kitabu cha Mwenyezi Mungu.
Bibi Maryam bint Saeed Al-Muhannadi, mkurugenzi wa kituo hicho, alisisitiza kuwa lengo kuu la mpango huu ni kufundisha Qur’ani Tukufu kwa mtazamo mpana unaovuka mipaka ya kuhifadhi na kusoma pekee, bali kusimika tabia, mwenendo na maadili ya Qur’ani katika maisha ya kila siku ya washiriki.
“Dira yetu ni kukifanya kituo hiki kuwa zaidi ya mahali pa kuhifadhi Qur’ani pekee; tunataka kukigeuza kuwa ‘Nyumba halisi ya Qur’ani’, mahali ambapo mtoto wa kike anakua akipenda Kitabu cha Mwenyezi Mungu, ambapo binti mdogo anaimarisha mafungamano yake na Qur’ani, na ambapo wanawake wanaweza kuendeleza safari yao ya kiroho na Kitabu kitukufu katika hatua mbalimbali za maisha yao.”
Bibi Al-Muhannadi aliongeza kusema: “Elimu ya Qur’ani Tukufu haikomi kwenye kuhifadhi aya; kinyume chake, taathira na matunda yake halisi huanza pale maana na tunu za Qur’ani zinapobadilika kuwa sehemu ya tabia, mwenendo mwema na mtindo mzima wa maisha ya muumini.”
Alibainisha zaidi: “Tutajitahidi kutoa programu bora na zenye viwango vya juu za Qur’ani na malezi, tukiwa na lengo la kufikia ufanisi wa hali ya juu katika elimu, malezi sahihi ya Kiislamu, na kuwa na athari chanya na yenye mashiko ya kudumu.”
Bibi Al-Muhannadi alihitimisha kwa kusema: “Tunapomfundisha mtu Qur’ani, hatulei tu mtu mwenye kuhifadhi Kitabu cha Mwenyezi Mungu (Hafidha), bali tunapanda mbegu ya thamani kubwa katika kizazi chote na kujenga taathira chanya inayoenea na kuinua familia nzima.”
3498863