IQNA

19:17 - September 01, 2026
Habari ID: 3482705

Balozi wa Iraq: Mpango wa ‘Saa ya Qur’ani’ nchini Malaysia unapaswa kufanyika kila mwezi

IQNA – Mwanadiplomasia mwandamizi wa Iraq ametoa wito na kueleza matumaini yake kuwa mpango wa kimataifa wa “Saa ya Qur’ani” (#QuranHour) utakuwa ukifanyika kila mwezi badala ya mara moja tu kwa mwaka.

Hudayfa Zead

Kaimu Balozi wa Ubalozi wa Jamhuri ya Iraq nchini Malaysia, Bw. Hudayfa Zead Mahmoud Salih, ameeleza kuwa mpango wa #QuranHour wa Malaysia unapaswa kuandaliwa kila mwezi ili kuwapa Waislamu fursa zaidi za kupanua na kuimarisha uelewa wao wa mafundisho na miongozo ya Kitabu Kitukufu cha Mwenyezi Mungu.

Alibainisha kuwa mikusanyiko na programu za namna hii zina umuhimu mkubwa mno, kwani Qur’ani Tukufu haikuteremshwa kuwa mwongozo wa ibada za faradhi pekee, bali inajumuisha na kuongoza nyanja zote za maisha ya mwanadamu.

"Matumaini yangu ni kwamba isiwe mara moja tu kwa mwaka. Natamani ingekuwa kila mwezi, kwa sababu maudhui na mafunzo ya Qur’ani ni mapana sana na yamebeba kanuni na sheria nyingi za maisha.

“Qur’ani si kwa ajili ya ibada au swala pekee; Qur’ani inajumuisha kila kitu; kutoa hekima, kuelekeza masuala ya uchumi na kusimamia mwenendo mzima wa maisha ya kawaida ya kila siku,” alieleza mwanadiplomasia huyo alipozungumza na gazeti la Sinar Harian wakati wa hafla ya mpango wa #QuranHour nchini Malaysia, iliyofanyika katika Msikiti wa Al-Sultan Abdullah, uliopo eneo la Presint Merdeka 118, siku ya Jumapili.

Aliongeza kusema kuwa vikao, halqa na programu nyingi zaidi zinazofungamana na Qur’ani zinapaswa kuandaliwa ili kuwawezesha waumini na jamii kwa ujumla kupata elimu ya kina na kufahamu vizuri zaidi uongofu na hekima zilizomo ndani ya Kitabu cha Mwenyezi Mungu.

Afisa huyo wa Iraq alisisitiza kuwa programu kama vile Malaysia #QuranHour hutumika kama jukwaa adhimu la kukuza uelewa wa umma kuhusu Qur’ani na kuhamasisha Waislamu kutekeleza na kuishi kwa kufuata mafundisho yake katika maisha yao ya kila siku.

“Ninaamini tunahitaji vipindi na mikusanyiko mingi ya namna hii ili kuwapa watu fursa ya kuijua zaidi Qur’ani na kuifanya sehemu ya maisha yao,” alihitimisha.

/3498853

captcha