IQNA – Hatua ya uvamizi na ukiukaji wa heshima ya Msikiti Mtukufu wa Al-Aqsa mjini Al Quds (Jerusalem) uliofanywa na waziri mwenye misimamo mikali ya Kizayuni, Itamar Ben-Gvir, akiongozana na makundi ya walowezi haramu wa Kizayuni chini ya ulinzi mkali wa vikosi vamizi vya utawala haramu wa Israel, imeibua lawama na ukosoaji mkali kutoka nchini Jordan.
Wizara ya Mambo ya Nje ya Jordan imelaani vikali uchokozi huo na kuutaja kuwa ni ukiukaji wa wazi wa hadhi ya kihistoria na kisheria ya Haram al-Sharif, kuvunjiwa heshima utakatifu wake, uchochezi uliopitiliza unaolaaniwa, na hatua ya uchokozi isiyokubalika kamwe.
Msemaji rasmi wa wizara hiyo, Balozi Fouad Majali, alithibitisha siku ya Jumatatu msimamo thabiti wa nchi hiyo wa kukataa katakata na kulaani vikali mwendelezo wa uvamizi unaofanywa na mawaziri, maafisa, na walowezi wenye itikadi kali za Kizayuni, pamoja na mienendo yao ya chokochoko. Alikemea pia usaidizi unaotolewa na polisi ya utawala ghasibu wa Kizayuni kufanikisha uvamizi huo wa kila uchao ndani ya Msikiti Mtukufu wa Al-Aqsa/Haram al-Sharif; akibainisha kuwa ni uvunjaji wa wazi wa sheria za kimataifa na sheria za kibinadamu, na ni jaribio batili linalolenga kulazimisha uhalisia mpya ndani ya eneo hilo takatifu kupitia njama za kutaka kuugawa msikiti huo kiwakati na kimaeneo (temporal and spatial division).
Balozi Majali alionya dhidi ya athari mbaya za kuendelea kwa uvamizi na ukiukaji wa maeneo matakatifu ya Kiislamu na Kikristo pamoja na kuvurugwa kwa hadhi iliyopo ya kihistoria na kisheria mjini Quds (Jerusalem) na maeneo yake matukufu, akisisitiza kwa msisitizo kuwa utawala ghasibu wa Israel hauna mamlaka yoyote ya kiutawala (sovereignty) juu ya mji unaokaliwa kwa mabavu wa Quds wala maeneo yake matakatifu ya Kiislamu na Kikristo.
Alikariri kuwa eneo lote la Msikiti Mtukufu wa Al-Aqsa, lenye ukubwa wa dunam 144, ni mahali patakatifu pa ibada mahususi kwa Waislamu pekee, na kwamba Idara ya Wakfu ya Quds na Masuala ya Msikiti wa Al-Aqsa, inayofungamana na Wizara ya Wakfu na Masuala ya Kiislamu ya Jordan, ndiyo chombo pekee chenye mamlaka ya kisheria na ya kipekee ya kusimamia masuala yote ya Msikiti Mtukufu wa Al-Aqsa/Haram al-Sharif na kuratibu taratibu zote za kuingia ndani yake.
Majali alitoa mwito kwa jamii ya kimataifa kuchukua msimamo thabiti na madhubuti wa kuushinikiza utawala huo ghasibu unaokalia ardhi hizo kwa mabavu kusitisha mara moja jinai na uvunjaji wa sheria dhidi ya maeneo matakatifu ya Kiislamu na Kikristo mjini Quds, pamoja na kukomesha chokochoko zote za viongozi na walowezi wa Kizayuni, ambazo zinaakisi sera hatari za utawala huo na upanuzi wa mashambulizi katika Ukingo wa Magharibi unaokaliwa kwa mabavu.
3498860