IQNA – Wizara ya Wakfu na Masuala ya Kiislamu ya Misri imeandaa semina 625 za kielimu zilizobeba anwani isemayo: “Mtume Mtukufu (SAW); Kielelezo Kamili na Ngao ya Maadili Mema,” zikifanyika katika mikoa ya mipakani ya nchi hiyo.
Semina hizo zilifanyika siku ya Jumatatu mara baada ya swala ya Isha katika ofisi na vituo mbalimbali vya Wakfu vilivyoko kwenye mikoa ya mipakani.
Mikusanyiko hii ya kielimu ni sehemu ya programu za wizara hiyo za kulingania dini (Dawah), kutoa elimu na kuamsha mwamko wa jamii, ikienda sambamba na mpango maalum uliopewa jina la “Sahihisha Mitazamo Yako”.
Lengo kuu la semina hizi ni kutoa mtazamo mpana na wa kina kuhusu Sira (wasifu na mwenendo) ya Bwana Mtume Muhammad (SAW), fadhila na tunu zake za kimaadili, pamoja na sifa tukufu alizozidhihirisha Mtume Mtukufu (SAW) katika uhai wake wote.
Semina hizo zimejikita katika kuangazia taathira chanya ya maadili mema katika ujenzi wa shakhsiya ya muumini na kuimarisha mafungamano ya kijamii, kwa shabaha ya kueneza misingi mizuri na kurekebisha fikra potofu pamoja na tabia zisizofaa.
Tukio hili ni sehemu ya mlolongo wa semina za kielimu za wizara hiyo zinazolenga kuinua hadhi na wajibu wa misikiti katika malezi na ulinganizi, pamoja na kuunganisha mimbari na khutba za kidini na masuala halisi yanayojenga uelewa na kuimarisha tunu za kiroho miongoni mwa wanajamii.
Kwa kuweka msisitizo kwenye Seerah na maadili matukufu ya Mtume (SAW) katika miamala yake na watu wengine, semina hizo zinafafanua mfano kamili na wa kiutendaji wa mwenendo wake katika kutenda wema, kuwa na huruma na upendo, kuheshimiana, na kushikamana kijamii.
Aidha, vikao hivyo vilisisitiza kuwa maadili ya Kinabii si nadharia au kanuni za kinadharia tu zinazokaririwa, bali ni mfumo kamili wa maisha kwa ajili ya kumjenga mwanadamu na kuunda jamii imara inayojengwa juu ya misingi ya kuheshimiana, huruma na ushirikiano—mambo yanayosaidia juhudi za kurekebisha tafsiri potofu na kuhimiza mienendo mizuri.
Semina hizi zinafanyika katika mikoa mbalimbali ya mipakani mwa Misri, ikijumuisha Bahari ya Shamu , Sinai Kusini, Wadi al-Jadeed, Matrouh, Sinai Kaskazini, na Suez.
3498861