IQNA

14:18 - September 02, 2026
Habari ID: 3482708

Mgogoro wa Rohingya: Mwaka wa tisa wa mateso, upungufu wa misaada, na matumaini yaliyofifia

IQNA – Mgogoro wa wakimbizi wa Rohingya umeingia katika mwaka wake wa tisa, huku zaidi ya watu milioni moja wakiwa wamekwama nchini Bangladesh bila matumaini ya wazi ya kurejea kwa usalama na hadhi nchini Myanmar.

Licha ya juhudi za kimataifa za miaka mingi, bado hakuna suluhu ya kisiasa inayozingatia haki za kimsingi, ikiwemo njia ya uhakika ya kupata uraia, wala hakuna hakikisho lolote la kuaminika kuwa wakimbizi hawa watapata usalama na uhuru wakirejea katika nchi yao.

Katika mahojiano na Al Jazeera, mwakilishi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi (UNHCR) nchini Bangladesh, Evo Freyen, alizungumzia hali inayozidi kuwa mbaya ya kibinadamu, kupungua kwa ufadhili wa kimataifa, mustakabali wa watoto wa Rohingya, na masharti muhimu yanayohitajika ili kurejea kwa wakimbizi hao nchini Myanmar kwa njia endelevu.

Ingawa Freyen alikataa dhana kuwa jumuiya ya kimataifa imewasahau kabisa Rohingya, akibainisha kuwa wafadhili wameendelea kutoa misaada kwa miaka mingi, alikiri kuwa ufadhili sasa unashuka huku idadi ya wakimbizi nchini Bangladesh ikiongezeka. Alisema kuwa asili ya muda mrefu ya mgogoro huu inawafanya wakimbizi wengi kuanza kuhoji ikiwa kurejea Myanmar kutawahi kuwezekana.

Ujumbe wake kwa jumuiya ya kimataifa ni kwamba nchi lazima zishirikiane, zifanye mazungumzo na wadau mbalimbali nchini Myanmar, na kufanya kazi ili kuunda mazingira ambayo yatawapa wakimbizi matumaini kwamba kurejea nyumbani kunawezekana.

Bangladesh, ambayo imewahifadhi wakimbizi hawa tangu wimbi kubwa la mwaka 2017 kufuatia ukandamizaji wa kijeshi katika Jimbo la Rakhine, imesisitiza kuwa haiwezi kubeba mzigo huu bila mwisho. Hali ya kibinadamu katika kambi za Cox’s Bazar inasalia kuwa tete sana, huku takriban asilimia 95 ya wakimbizi wakitegemea misaada ya kibinadamu kwa mahitaji yao yote.

Wasiwasi mkubwa sasa ni kwa watoto wa Rohingya, ambao wengi wao wanakua katika kambi bila hadhi ya kisheria, fursa ndogo za elimu rasmi, na vizuizi vya uhuru wa kutembea, hali ambayo inatishia kuzalisha “kizazi kilichopotea” (lost generation) ambacho hakina mustakabali wa uhakika.

/3498877

Kishikizo: rohingya waislamu
captcha