IQNA – Kila mwaka, mamilioni ya Waislamu husafiri kwenda Makka na Madina kwa ajili ya Hija na Umra, na kila mwaka, masuala ya uratibu wa usafirishaji, afya, na udhibiti wa umati huleta changamoto kubwa.
Sasa, zaidi ya waombaji 400 wamejiunga na Hajjathon ya nne, mpango wa uvumbuzi unaolenga kuandaa suluhisho za kivitendo ili kuboresha huduma kwa mahujaji wa Hija na Umra pamoja na wageni.
Hatua ya kwanza ya Hajjathon, iliyofanyika kama sehemu ya Kongamano la 26 la Kisayansi la Utafiti wa Hija, Umra na Ziyara, ilivutia waombaji 405, wakiwemo wanawake 304 na wanaume 101.
Teknolojia na akili mnemba (AI) vilikuwa vichocheo maarufu zaidi kati ya njia nne za ushindani, vikivutia maombi 168, ikifuatiwa na sekta ya afya kwa maombi 144. Njia ya uhamasishaji na udhibiti wa umati ilipokea maombi 69, huku uhandisi na miundombinu ikirekodi maombi 24.
Kampuni ya Wadi Makkah Technology, ambayo ni tawi la uwekezaji la Chuo Kikuu cha Umm Al-Qura, inashiriki kama mfadhili wa uvumbuzi wa kongamano hilo. Kampuni hiyo ilisema ushiriki wake unalenga kusaidia kuendeleza mawazo bunifu kuwa miradi na suluhisho stahiki, ambazo zinaweza kuimarisha mfumo wa huduma za Hija na Umra na kuboresha uzoefu wa mahujaji na wageni.
Pia inatafuta kukuza matumizi ya teknolojia ibuka na akili mnemba katika kuendeleza huduma hizo.
Kongamano hilo litaandaliwa na Chuo Kikuu cha Umm Al-Qura kupitia Taasisi ya Mlinzi wa Misikiti Miwili Mitakatifu kwa Utafiti wa Hija na Umra mnamo Septemba 2 na 3 chini ya kaulimbiu “Ubora na Ushirikiano katika Mfumo wa Huduma za Hija na Umra.”
3498869