IQNA – Mwanamke mmoja wa Kimisri mwenye umri wa miaka 71 amefanikiwa kukamilisha Khatm Qu'ran (kusoma Qur’ani nzima) kwa siku moja pekee.
Hajiya Sana Abdel Sattar anatokea kijiji cha Meit Shahala katika mkoa wa Menoufia. Yeye ni mfano halisi wa azma thabiti na uhusiano wa kina na Qur’ani Tukufu.
Amefanikiwa kusoma Qur’ani nzima kwa siku moja (katika kikao kimoja), kuanzia wakati wa baada ya swala ya alfajiri mpaka wakati wa machweo (Maghrib).
Nyuma ya mafanikio haya ya kupongezwa kuna safari ndefu iliyoanza miongo mingi iliyopita, wakati Hajiya Sana alipokuwa akijenga uhusiano wa karibu na Qur’ani Tukufu akiwa katika miaka yake ya mapema ya ishirini, huku Shirika la Redio la Qur’ani likiwa dirisha lililofungua njia ya kumkaribisha kitabu hiki kitukufu ndani ya moyo wake.
Hajiya Sana anasema kuwa alianza kusoma na kuhifadhi Qur’ani akiwa kijana. Alianza safari hii kwa sababu alikuwa akisikiliza Redio ya Qur’ani mara kwa mara.
“Ilikuwa zawadi kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Nilihifadhi Qur’ani nikiwa katika miaka yangu ya mapema ya ishirini. Kusikiliza Redio ya Qur’ani kulinijengea upendo kwa kitabu hiki kitukufu na azma ya kukihifadhi.”
Aliendelea na safari ya kuhifadhi huku akiwa amekabiliwa na majukumu ya maisha ya ndoa na kulea watoto. Hajiya Sana ni mama wa wanaume watatu: Muhammad (miaka 50), Mahmoud (miaka 45), na Mustafa (miaka 42), ambaye ni mfamasia.
Licha ya shughuli nyingi za nyumbani na kulea watoto, kila wakati alijitahidi kutenga muda kwa ajili ya Qur’ani lakini safari hii ilikatizwa kutokana na ugonjwa wa mumewe.
Hajiya Sana alisitisha mchakato wake wa kuhifadhi Qur’ani wakati wa kipindi cha miezi sita cha ugonjwa wa mumewe ili kumtunza. Baada ya kifo cha mumewe, pia alipitia kipindi kigumu kilichomzuia kuendelea na safari yake ya kuhifadhi Qur’ani.
Hata hivyo, usitishaji huo haukuwa mwisho wa safari yake. Hatimaye, Hajiya Sana alirejea kwa Qur’ani na kutafuta mtu wa kumsaidia kuihifadhi na kuirejelea (mushafadha).
Moja ya kilele cha safari ya Qur’ani ya Hajiya Sana kilikuwa ushiriki wake katika kikao cha kusoma Qur’ani; alianza kusoma kutoka kichwani baada ya swala ya alfajiri na kuendelea mpaka machweo, hivyo kufanikiwa kuisoma Qur’ani Tukufu nzima.
/3498866/