IQNA – Kampuni ya mavazi ya michezo ya Adidas inakabiliwa na wimbi kubwa la kususwa na watumiaji wiki hii, huku wanaharakati na watumiaji wa mitandao ya kijamii wakitoa wito wa kuacha kununua bidhaa za kampuni hiyo kutokana na kampeni ya kimataifa ya matangazo ambayo inamuonyesha waziwazi mwanajeshi katili wa Israel aliyeko kazini.
Wito wa kususia Adidas unaendelea kukua baada ya kampuni hiyo kumtumia mwanajeshi huyo katika kampeni zake. Kampeni hiyo imeibua ukosoaji mkali kutoka kwa mashirika na wanaharakati wanaoiunga mkono Palestina kwa sababu ya ushiriki wa mwanajeshi huyo, Shaliv Biton, katika mauaji ya kimbari yanayofanywa na utawala wa Israel dhidi ya watu wa Gaza.
Biton alishiriki katika shambulio la Israel huko Gaza mnamo 2021 ambalo lilisababisha vifo vya zaidi ya Wapalestina 200 na kuharibu majengo mengi. Wakosoaji wamekumbusha historia ya kijeshi ya Biton na shughuli zake katika mitandao ya kijamii, ambapo amekuwa akishiriki picha na video zake na wanajeshi wengine wa Israel wakiwa Gaza, zikiwemo picha za wanajeshi hao wakiimba na kucheza, huku wasifu wake pia ukiwa na picha zake akiwa amebeba silaha.
Mwandishi wa habari za michezo, Leyla Hamed, aliikosoa Adidas kwa chaguo lake la mwakilishi wa kampeni, akibainisha kuwa kampuni hiyo ilichagua kutumia hali ya Biton ya kupoteza mguu kwa ajili ya faida za kibiashara, wakati ilipaswa kuzingatia muktadha mpana zaidi wa watu waliopoteza viungo Gaza.
“Gaza ina kiwango cha juu zaidi cha watoto waliokatwa viungo duniani. Zaidi ya 5,000 wamekatwa viungo tangu Oktoba 2023, kutokana na mashambulizi ya Israel yaliyofanywa na wanajeshi kama huyu ambaye Adidas imemchagua kuwa mfano wao,” aliandika kwenye X.
Mchambuzi wa kisiasa na mwanaharakati nchini Marekani, Guy Christensen, pia alilaani kampeni hiyo akisema, “Inachukiza sana unapojua kuna watoto huko Gaza ambao huenda wasiweze kutembea tena milele.” Wanaharakati wengine wamelaani Adidas kwa kujihusisha na utawala unaotekeleza mauaji ya kimbari na ubaguzi wa rangi (apartheid).
3498900
Zenye maoni mengi zaidi