IQNA – Kinachotofautisha mtindo wa Misri wa Qira’a na harakati nyingine za qiraaa au usomaji Qur'ani Tukufu, hasa mitindo inayozidi kupata umaarufu katika ukanda wa Ghuba ya Uajemi, ni uhusiano wa kina ambao maqari (wasomaji) wa Misri wameujenga kati ya kanuni na mafundisho ya kusoma Qur’an Tukufu na uelewa sahihi wa maqamat (mitindo ya sauti) za kimuziki.
Ingawa Misri ndiyo chimbuko asili la fani ya Qira’a katika ulimwengu wa Kiislamu, katika mazingira ya sasa ya vyombo vya habari tunashuhudia “kusahaulika kwa taratibu mtindo halisi” na “kuvunjika kwa uhusiano kati ya kizazi kipya cha maqari na urithi wa waliotangulia.”
Leo, baadhi ya Qira’a za kibiashara na zisizo na kina zimechukua nafasi ya Qira’a za kitaalamu na zinazochochea fikra. Aidha, mbinu sahihi za Waqf (kusimama), Ibtida (kuanza), lahn, sauti, na Tajweed, ambavyo ni matokeo ya uzoefu wa karne nyingi wa mabingwa wa Misri, hazihifadhiwi wala kufundishwa ipasavyo.
Katika mfululizo wa taarifa, Shirika la Habari za Qur'ani la Kimataifa (IQNA), linalenga kurejelea mageuzi ya fani hii, kuanzia “mtindo au shule ya zamani” hadi kujitokeza kwa “mabingwa wa Qira’a,” huku ikitathmini hali ya sasa, ili kujenga daraja kati ya mbinu asili za Misri na mahitaji ya kisanii ya hadhira ya Qur’an ya leo. Lengo ni kurudisha fani ya Qira’a kutoka katika “ibada ya kuiga tu” na kuifanya kuwa “mtiririko hai na wenye nguvu.”
Hii ni kwa sababu Qira’a zenye utukufu za leo zinatokana na shule ya kimapokeo ya Misri, na kuelewa mchakato huu wa kihistoria ni muhimu ili kuelewa uhalisia wa Qira’a. Pia, kwa kufuata mfano wa kisanii, kuwatambulisha mapainia wa Misri na mbinu zao ni mfano bora kwa qari vijana ili kuboresha viwango vya kiufundi na kiroho vya Qira’a yao.
Shule ya Misri ya Qira’a ya Qur’an ni sawa na jengo kubwa lililojengwa na maqari mashuhuri katika vizazi kadhaa. Kinachoiweka shule ya Misri tofauti na mitindo mingine ya Qira’a, hasa ile inayozidi kupata umaarufu katika miongo ya hivi karibuni kupitia mitandao ya kijamii na satelaiti katika ukanda wa Ghuba ya Uajemi, ni uhusiano wa ndani uliopo kati ya misingi ya kusoma Qur’an na uelewa wa kina wa maqamat.
Hali hii haina uhusiano na kuimba au kujifunza vyombo vya muziki, bali ni uelewa wa qari kuhusu uwezo wa sauti yake na koo lake, na jinsi ya kuzielekeza katika kutoa maana za aya za Qur’an Tukufu. Hii huambatana na heshima, khofu, na matumaini ya msaada wa Mungu, ushindi, na peponi wakati wa Qira’a, jambo ambalo mabingwa wa shule ya Misri walilielewa vyema na hata kufanikiwa kwa kiasi kikubwa, iwe kwa asili au kwa kujifunza na mazoezi.
Wengi wa maqari wakuu wa Misri walipenda sana elimu ya sauti na mitindo ya maqamat kwa weledi. Kwa mfano, Sheikh Muhammad Rifaat alikuwa akisikiliza kazi za Beethoven na Mozart, huku Sheikh Mahmoud al-Banna akijifunza maqamat kitaalamu chini ya Sheikh Darwish al-Hariri, ambaye alikuwa mwalimu wa muziki wa Muhammad Abdul-Wahhab.
Hata wasanii kama Abdul-Wahhab au Umm Kulthum walikuwa wakitafuta qari ili kujifunza sanaa ya sauti na maqamat, na walikuwa na uhusiano wa karibu na baadhi ya masheikh hili.
Taha Muhammad Abdul Wahab alikuwa mtaalamu wa maqamat na sauti, mwamuzi wa kimataifa nchini Misri na ulimwengu wa Kiarabu, na alikuwa na shahada ya uzamili katika maqamat za Qur’ani na aliwafundisha qari wengi mashuhuri.
Sheikh al-Qurra Muhammad Rifaat alijulikana kwa sauti yenye nguvu, ya kipekee, na inayobadilika kwa urahisi; aliweza kusoma aya kwa urahisi na kwa nafasi sahihi za kimuziki, jambo lililomfanya msomaji ajihisi kana kwamba aya ya Qur’an imeshuka mbele yake.
Kwa upande mwingine, sauti ya Sheikh Abdul Basit Abdul Samad, ikiwa na huzuni yake ya kipekee na unyenyekevu, inang’ara zaidi katika maqam ya Saba. Kutokana na nguvu ya sauti yake na athari ya Qira’a yake, mkurugenzi marehemu Mustafa Akkad alitumia sauti ya Sheikh Abdul Basit katika filamu yake maarufu “The Message” kama sauti ya Bilal al-Habashi, muadhini wa Mtume (SAW). Adhana hiyo ilikuwa ya kipekee kutokana na ubora wa kustaajabisha wa sauti ya Abdul Basit.
3498905
Zenye maoni mengi zaidi