IQNA

11:36 - September 06, 2026
Habari ID: 3482727

Msahafu unaonasibishwa na  Imam Ali (AS) waonyeshwa katika Maonyesho ya Vitabu ya Baghdad

IQNA – Banda la Idara ya Ataba (Haram) Tukufu ya Imam Ali (AS) limeweka wazi nakala ya muswada wa Qur’an Tukufu inayohusishwa na Imamu huyo katika Maonyesho ya 27 ya Kimataifa ya Vitabu ya Baghdad.

b

Idara ya Masuala ya Kifikra na Kitamaduni ya Ataba hiyo imeshiriki kikamilifu katika maonyesho hayo ya mwaka huu, ikiwa na banda maalum lililoandaliwa kwa uzuri na lenye maudhui mazito ya kiutamaduni na kielimu kwa wageni.

Ammar Mashallah, naibu mkuu wa idara hiyo, alieleza kuwa banda hilo lina zaidi ya kazi 300 tofauti zilizozalishwa na idara yao, zinazogusia nyanja mbalimbali za kiakili, kitamaduni, na urithi wa Kiislamu. Alibainisha kuwa hatua hii inalenga kutambulisha bidhaa za kisayansi na kiakili zinazoandaliwa na Ataba hiyo.

Sehemu moja ya kuvutia sana katika banda hilo ni ukuta wa Nahj al-Balagha, wenye eneo la zaidi ya mita za mraba 18. Ukuta huo una mpango wa kina wa kutambulisha matoleo muhimu zaidi ya Nahj al-Balagha na ufafanuzi wake mashuhuri, ukisisitiza hadhi ya kazi hii ya milele na umakini wa kielimu na utafiti ulioelekezwa kwake katika kipindi chote cha historia.

“Pia, katika banda hili, kuna mkusanyo wa magazeti na majarida ya zamani ya Najaf yaliyochapishwa tangu mwaka 1910. Miongoni mwa machapisho haya ni Al-Ilm, Al-I’tidal, Al-Hira na Al-Bayan, pamoja na machapisho mengine muhimu yanayoakisi sehemu ya historia ya harakati za kitamaduni na vyombo vya habari vya mji huu mtakatifu,” aliongeza Mashallah.

Vilevile, mkusanyiko wa miswada muhimu zaidi ya mwandishi wa hati (khatati) mashuhuri marehemu Jassim Najafi unaonyeshwa kutokana na thamani yake ya kisanaa na kihistoria.

Kuhusu kazi nyingine adimu, Mashallah alisisitiza kuwa banda hilo limepambwa kwa kuonyeshwa kwa Msahafu au nakala ya Qur’an Tukufu inayohusishwa na Amiri wa Waumini (AS). Msahafu huu unachukuliwa kuwa moja ya miswada muhimu zaidi ya hazina ya Alawi, na imepata mapokezi makubwa kutoka kwa wageni wa maonyesho hayo kutokana na thamani yake kuu ya kidini, kihistoria, na kiurithi.

Maonyesho ya 27 ya Kimataifa ya Vitabu ya Baghdad yalianza Jumatano, Septemba 2, 2026, yakishirikisha zaidi ya wachapishaji 600 kutoka nchi 28, na yataendelea hadi Septemba 12.

3498897

Kishikizo: msahafu imam ali as iraq
captcha