IQNA – Sherehe kubwa imefanyika katika mji wa Hakkari, nchini Uturuki, kwa ajili ya kuwaenzi wahifadhi 300 wa Qur’an Tukufu.
Kikundi hiki cha wahifadhi wa Qur’ani Tukufu, ambao wamemaliza vyema safari yao ya kuweka akilini mwao kitabu hicho kitukufu kwa ukamilifu, kilipewa heshima katika hafla iliyoandaliwa katika Msikiti wa Chuo Kikuu cha Hakkari, kwa mujibu wa ripoti ya newturkpost.
Hafla hiyo ilifanyika siku moja baada ya kumalizika kwa raundi ya fainali ya shindano la kuhifadhi Qur’ani Tukufu la Uturuki, ambalo mji wa Hakkari ulikuwa mwenyeji wake. Sherehe hiyo ilijawa na baraka za usomaji wa aya za Qur’ani, utenzi wa kasida, na dua.
Naibu Gavana wa Hakkari, Orcun Cünit Zur, alihutubia hadhira hiyo na kusisitiza kuwa matukio haya mawili, fainali ya shindano la Qur’ani na mahafali ya wahifadhi, ni ishara ya mustakabali mwema kwa mji wa Hakkari na nchi nzima ya Uturuki.
Aliwapongeza wahifadhi hao akisema: “Ninawapongeza kwa dhati nyinyi vijana mliofanya kazi mchana na usiku ili kuhifadhi Qur’ani Tukufu. Mmeanzisha safari yenye maana kubwa na nzuri sana. Namuomba Mwenyezi Mungu afanye njia yenu kuwa nyepesi na atuthibitishie elimu na maadili yenu.”
Naye İsrafil Kışla, Mshauri Mkuu wa Rais wa Uturuki, alipata fursa ya kutoa hotuba na kuonyesha furaha yake kubwa kwa kushiriki katika hafla hiyo ya kihistoria.
Akizungumza na wazazi, Kışla alisema: “Huu ni hisia ya ajabu sana kwetu. Nawapongeza wazazi. InshaAllah, watoto wenu watakuwa chanzo cha fahari kwenu katika maisha ya akhera.”
Aliongeza: “Hatupaswi kuwasahau walimu wetu, kwa sababu mbora wenu ni yule anayejifunza Qur’ani na kuifundisha. Namuomba Mwenyezi Mungu abariki maisha yenu, Qur’ani iwe nanyi hadi mwisho wa maisha yenu, na maisha yenu yawe yameongozwa na maadili ya Qur’ani na mwenendo wa Mtume Muhammad (SAW).”
3498910
Zenye maoni mengi zaidi