Katika mazingira ya kiroho yaliyojaa baraka, Haram Tukufu ya Hadhrat Abbas (AS) mjini Karbala, Iraq, imeandaa hafla ya kila wiki ya Qur’an inayojulikana kama “Arsh ya Qira’a” (Mbingu ya Usomaji).
Tukio hili liliandaliwa na Idara ya Kisayansi ya Qur’an ya Astan (Usimamizi wa Haram), likiwaleta pamoja wanafunzi wanaoshiriki katika toleo la kumi la mradi wa kitaifa wa “Amir al-Qurra” (Mfalme wa Wasomaji).
Ali al-Fatimi, mmoja wa maafisa wa idara hiyo ya Qur’ani, alibainisha kuwa mkusanyiko huu ulipambwa kwa ushiriki wa wasomaji mahiri na wanafunzi wa mradi wa “Amir al-Qurra”, sambamba na wasomaji rasmi wa Haram ya Abbas (AS). Aidha, kundi kubwa la mahujaji waliofika katika Haram hiyo walipata fursa ya kushiriki katika mpango huu wa kiroho, wakisikiliza aya tukufu zikirejelewa kwa ustadi wa hali ya juu na kwa kufuata kanuni za Tajweed.
Akizungumzia malengo mapana ya mradi huo, al-Fatimi alieleza kuwa mradi wa kitaifa wa “Amir al-Qurra” unajumuisha mfululizo wa programu za kielimu na shughuli zinazokusudia siyo tu kukuza elimu ya Qur’an, bali pia kuimarisha maadili na mafundisho ya kidini. Idara ya Kisayansi ya Qur’an ya Astan inaendelea kuandaa mikusanyiko hii kwa lengo la kupanua utamaduni wa Qur’an katika jamii, kuwahamasisha wasomaji (Maqari) kuendeleza sanaa ya kurejea neno la Allah, na kueneza sayansi na elimu ya Qur’ani kwa vizazi vya sasa na vijavyo.
3498930
Zenye maoni mengi zaidi